Balozi Seif: Ipo haja ya kuandaliwa mikakati ya muda mrefu ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza wakati wa Mvua.

Tathmini hiyo imekuja kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha
katika Maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba na kuathiri
Nyumba 325 Mkoa Kusinin Pemba, Nyumba 667 kuhamwa ndani ya Mkoa Mjini
Magharibi pamoja na kubomoka kwa miundombinu ya Bara bara na baadhi ya
Madaraja hasa Kisiwani Pemba.
Akitoa Taarifa za awali za athari ya mvua zilizojitokeza kwa mwaka wa
2017 tokea kuanza kwa msimu wa Mvua za Masika, Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Ali Juma Hamad alisema
athari ya Mvua hizo zimesababisha maporomoko ya ardhi yaliyosababisha
kufukia kwa baadhi ya Nyumba na Bara bara.
Nd. Ali alisema ziara za Viongozi wa Serikali zimegundua athari kubwa
ya uharibifu wa miundombinu ya Bara bara na nyumba kutokana na mvua
hizo hasa katika Mkoa wa Kusini Pemba na kusababisha kifo cha Mtoto
Mmoja Ramadhan Mohamed baada ya kuangukiwa na ukuta wa Madrasa Chanjani
Chake Chake Pemba.
Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar
Nd. Mohamed Khamis Ngwali alisema bado Visiwa vya Unguja na Pemba viko
katika msimu wa mvua hali ambayo wananchi wanapaswa kufuatilia Taarifa
zainazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa.
Nd.Ngwali alisema viwango vya mvua katika visiwa vya Zanzibar
viongezeka kama vilivyotangazwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
mnamo Tarehe 28 Mwezi uliopita na kuanza kunyesha mara moja siku
iliyofuata.
Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Kinga Wizara ya Afya Dr.Fadhil
Abdulla alieleza kwamba Wizara ya Afya tayari imeshajiandaa na
changamoto yoyote inayoweza kujitokeza endapo kutaibuka kwa maradhi ya
mripuko katika kipindi hichi cha msimu wa mvua za masika.
Dr. Fadhil alisema udhibiti wa vyakula vinavyouzwa katika maeneo ya
wazi bado mgumu na ndio uliochangia kuibuka kwa maradhi ya Kipindupindu
mwaka jana kwa asilimia 16%.
Alisema katika kukabidhiana na udhibiti wa mfumko wa maradhi ya
kuambukiza Wataalamu wa Afya tayari wameshapima wagonjwa 22
walioonyesha ishara ya kusumbuliwa na maradhi ya matumbo ya kuharisha.
Dr. Fadhil alitanabaisha wazi kwa jamii kwamba suala la matumizi bora
ya maji safi na salama ndio jambo la msingi litakalosaidia kujikinga
na maradhi ya kuambukiza ikiwemo kipindupindu.
Wakichangia mjadala huo baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya
Kukabiliana na Maafa Zanzibar walisema upo umuhimu wa wataalamu
kuendelea kutumia vyombo vya habari katika kuwaelimisha wananchi juu ya
kujikinga na maradhi mbali mbali.
Walisema suala la kutibu maji kwa kuyatia dawa ni jambo la msingi kwa
vile chanzo cha magonjwa ya miripuko ukiwemo ule wa hatari wa kuharisha
ni matumizi mabaya ya maji yasiyo salama.
Akiahirisha Kikao hicho Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi alisema ipo haja ya kuandaliwa mikakati ya muda mrefu ya
kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kila mwaka wakati wa msimu wa
mvua za Masika.
Balozi Seif alisema mpango wa kutibu maji safi na salama kabla ya
matumizi ya binaadamu linafaa kuzingatiwa ili kusaidia kujikinga na
maradhi yanayosababishwa na maji.
Alieleza kwamba elimu ya Afya iendelee kutolewa na Wataalamu wa afya
itakayokwenda sambamba na kujiepusha na viashiria vyote vinavyosababisha
kupata maradhi ya mripuko ikiwemo ulaji wa vyakula ovyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Serikali Kuu
inaangalia utaratibu wa namna inavyoweza kuwasaidia Wananchi ambao
nyumba zao zimeharibika kabisa kutokana na mafuriko ya Mvua.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar
9/5/2017.
chanzo: zanzibar24.
Comments