WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi Msaidizi wa Pembejeo
wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bw. Shenal Nyoni ili kupisha
uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili kwa kuongeza gharama za pembejeo kwa
kushirikiana na baadhi ya mawakala wa pembejeo za kilimo.
Amesema
Serikali italipa madeni yote ya mawakala wa pembejeo za kilimo mara
baada ya kukamilisha uhakiki na kujiridhisha juu ya uhalali wake, sababu
bado inawahitaji mawakala ili kushirikiana nao katika kuhudumia
wakulima kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumatatu, Aprili 10, 2017) katika kikao
alichokiitisha kwenye Makazi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma kati yake na
mawakala wa pembejeo za kilimo pamona na Maofisa kutoka Wizara ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
“Gharama
ya madeni ni kubwa kuliko pembejeo zilizosambazwa. Hii inatokana na
udanganyifu mkubwa unaofanywa na mawakala kwa kushirikiana na watendaji
wa Serikali wanaohusika na masuala ya pembejeo,”
Amesema
kuwa kwenye eneo la pembejeo kuna matatizo makubwa kutokana na baadhi
ya Maofisa kuzungumza na mawakala na kuongeza gharama za pembejeo kwa
lengo la kuibia Serikali na kisha kugawana fedha.
“Sasa
Serikali haiwezi kulipa madeni ya kutengenezwa bali tutawalipa stahili
zenu baada ya uhakiki kukamilika kama nilivyosema awali,”.
Waziri
Mkuu aliongeza mawakala wa pembejeo waliwasilisha Serikali deni la sh.
bilioni 65.4 kwa huduma waliyoitoa katika mikoa 25 ambapo Wizara ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi imekamilisha uhakiki wa madeni hayo kwa mikoa 10
ya Morogoro, Iringa, Njombe, Ruvuma, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma,
Kilimanjaro na Arusha ambayo madeni yake ni asilimia 70 ya madeni yote.
Alisema
ripoti ya uhakiki wa mikoa nane kati ya 10 imetoka (imebaki Katavi na
Kigoma) na kubainisha kuwa mikoa hiyo inadai sh. bilioni 36 kati ya hizo
sh. bilioni 11 bado zinaendelea kuhakikiwa, sh. bilioni 14 zimekataliwa
hivyo siyo madeni halali, sh. bilioni 8.2 ndiyo deni halali na sh.
bilioni 2.3 zinachungizwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU).
Waziri
Mkuu alisema uhakiki wa madeni kwa mikoa 15 iliyobakia ambayo madeni
yake ni asilimia 30 unaendelea ambapo amewasihi mawakala hao kuwa
wavumilivu katika kipindi ambacho Serikali inafanya uhakiki kwa kuwa
inataka itende haki kwa kila mtu kulipwa deni lake kwa kiwango
kinachostahili na watakaobainika kufanya udanganyifu watachukuliwa hatua
za kisheria.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.L.P 980, DODOMA
JUMATATU, APRILI 10, 2017.
chanzO:Mpekuziblog.
Comments