Tunzeni miundombinu ya barabara -Mbarawa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akisaidia kuchomeka vyuma katika daraja kubwa la Mto Nduruma lililopo kwenye barabara kuu inayounganisha mji wa Arusha- Holili-Voi lililopo kwenye ujenzi alipofanya ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi wa miundombinu katika miji ya Arusha na Manyara. (Picha na Ujenzi).SERIKALI imewataka wananchi kutunza na kuilinda miundombinu ya barabara na kuwaonya wale wote watakaohusika kuihujumu na kuiharibu, watashughulikiwa kwa kuwa watakuwa wamekosa uzalendo.

Agizo hilo limetolewa kwa nyakati tofauti na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, wakati akikagua ujenzi wa barabara za Sakina – Tengeru yenye urefu wa kilometa 14.1 na Southern bypass yenye urefu wa kilometa 42.5 ambazo kwa pamoja zimegharimu kiasi cha Sh bilioni 132.3.


Profesa Mbarawa alipotembelea barabara ya kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) hadi Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara yenye urefu wa kilometa 27, alisema serikali imetumia fedha zake za mapato ya ndani kiasi cha Sh bilioni 32.2.

Alisema serikali inatumia gharama kubwa kujenga barabara hizo ili zisaidie kurahisisha shughuli za kila siku za maendeleo na kuharakisha kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa kila mwananchi anao wajibu wa kuzilinda barabara na madaraja na kuyatunza kwa kujali alama na mipaka yake.

Akizungumza katika Mji wa Mirerani, Profesa Mbarawa alisema pamoja na eneo hilo kuwa na madini ya vito, lakini tangu dunia iumbwe hawakuwahi kupata barabara ya lami, lakini Serikali ya Awamu ya Tano imewajengea na iko karibu kukamilika.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Arusha, Mgeni Mwanga aliwataka wananchi waendelee kuwa wavumilivu wakati miradi hiyo ikiendelea hasa pale kunapojitokeza changamoto mbalimbali ikiwemo kuzifunga barabara kwa muda.
chanzo:Habarileo.

Comments