
Hayo aliyasema leo huko katika ukumbi wa zamani wa
Baraza la Wawakilishi katika hafla ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa
skuli za Mikoa ya Unguja na Pemba vilivyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo
la Uzini, Mohammed Raza Dharamsi kwa ajili ya mashindano maalum ya
‘UMOJA CUP’ chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa Serikali inatambua kuwa
katika maisha ya mwanaadamu yoyote michezo ina umuhimu, kwani huleta
mshikamano, kujuana, huburudisha na husaidia katika kujenga afya ya
akili na kiwiliwili kwa vijana na watu wazima.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza historia ya michezo hapa
nchini ikiwa ni pamoja na michezo katika skuli ambapo hata yeye mwenyewe
binafsi alishiriki kikamilifu wakati huo huku akisisitiza kuwa michezo
hudumisha umoja, udugu na kukuza ujasiri ambapo kwa hivi karibuni,
michezo imekuwa ni chanzo kikubwa cha ajira.
Aliongeza kuwa pamoja na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kuendeleza michezo na utamaduni katika Skuli lakini katika miaka
michache iliyopita hamasa ya michezo katika skuli ilionekana kushuka.
Hivyo, baada ya kuona hivyo alichukua juhudi za makusudi kutokana na
ukereketwa wake wa michezo alichukua hatua kadhaa ikiwemo kuwaita
wanamichezo mahiri wa zamani na wenye uzoefu mkubwa na kufanya nao
mazungumzo kwa lengo la kurejesha na kuinua sekta ya michezo hapa
nchini.
Alieleza kuwa miongoni mwa hatua za awali alizozichukua ni kuanzisha
kwa Idara ya Michezo na Utamaduni katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Amali, kuazisha mashindano ya riadha ya Wilaya, kugawa vifaa pamoja na
mambo mengineyo.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa katika kuendeleza na kuimarisha
shughuli za michezo na utamaduni katika skuli, Serikali itaendelea
kutilia mkazo utekelezaji wa mipango ya kuimarisha michezo na sanaa
ukiwemo Mpango wa Sport 55 na kupongeza hatua hiyo.
Akielez mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuimarisha sekta ya michezo alisema kuwa Serikali ina mpango wa kujenga
uwanja mpya utakaochukua watu 45,000 kwa wakati mmoja huko katika mji
mpya wa Fumba sambamba na imeshaamua kujenga kiwanja kimoja cha michezo
katika kila Wilaya Unguja na Pemba na tayari kiwanja kilichopo katika
Wilaya ya Kusini huko Kitogani kimeshakuwa tayari.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Mwakilishi wa Jimbo
la Uzini Mohammed Raza kwa upendo na uzalendo wake huo wa kuendelea
kuunga mkono maendeleo ya sekta mbali mbali nchini ikiwemo sekta ya
michezo na kupelekea kutoa vifaa hivyo kwa Wizara ya Elimu vikiwemo
jezi, mipira, viatu, soksi, kikombe, medali za dhahabu na fedha,
shinguard na vifaa vyenginevyo.
Pia, alitoa pongezi kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa
kuendelza sekta hiyo huku akitoa wito kwa Wizara hiyo kuangalia
uwezekano wa kuanzisha mashindano katika skuli za msingi na Sekondari
hasa mashindano kwa kutumia ‘Inter houses’.
Nae Waziri wa Elimu an Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma
alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuanzisha Idara ya Michezo na Utamaduni
katika Wizara hiyo hatua ambayo imepelekea kuhamasika kwa michezo na
kuaza kwa vuguvugu la michezo kama ilivyokuw kwa siku za nyuma.
Aidha, alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Mwakilishi wa
Jimbo la Uzini, Mohammed Raza kwa hatua yake hiyo ya kuonesha
mashirikiano makubwa kwa Serikali pamoja na Wizara hiyo ya Elimu na
kumsifu kuwa ni kionozi anaetekeleza ahadi zake kwa vitendo.
Nae Mohammed Raza alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa ataendelea
kuiunga mkono Serikali katika kuendeleza sekta mbali mbali za maendeleo
kwa kutoa misaada yake na kueleza kuwa ahadi zake zote alizoziahidi
atazitekeleza.
Aliongeza kuwa juhudi hizo anazozichukua ni katika kutekeleza Ilani
ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ambayo imesisitiza kuimarishwa kwa
michezo, hivyo akiwa kiongozi na mkerekwetwa katika sekta hiyo ni vyema
kuiendeleza na kuiimarisha sekta hiyo hapa nchini.
Pia, aliwaeleza wanafunzi ambao ndio walengwa wa vifaa hivyo kuwa
mbali ya kucheza michezo mbali mbali katika skuli zao pia, ni vyema
wakajua historia yao sambamba na kutambua mafanikio yaliopatikana
kutokana na Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Sambamba na hayo, Raza aliahidi kutoa vifaa kwa ajili ya mashindano
ya netiball kwa skuli za Unguja na Pemba huku akisisitiza ahadi yake ya
kuzihudumia timu mbili za Mkoa wa Kusini na Kaskazini Pemba
zitakazokuja katika mashindano hayo hapa Unguja ambapo gharama zote za
vifaa pamoja na huduma hiyo zitafikia milioni 25..
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khadija
Bakari alisema kuwa Wizara imeelekeza nguvu zake katika usimamizi na
utekelezaji thabiti wa shughuli zote za elimu zikiwemo utekelezaji wa
Mpango wa ‘Sport 55’ unaolenga kuimarisha michezo katika skuli.
Aidha, aliongeza kuwa mikakati maalumu imeandaliwa na itatekelezwa
kuanzia ngazi za skuli katika kurejesha shughuli zinzowajenga wanafunzi
kuwa wakakamavu, wenye nidhamu na maadili mema, wanaofahamu mila, silka
na desturi njema za Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Comments