Serikali kuweka mazingira wezeshi kutibu maji.

SERIKALI imesema ipo tayari kushirikiana na taasisi za Korea zilizokuja na teknolojia mpya ya kutibu maji kwa kuweka mazingira wezeshi ili kutimiza malengo ya serikali ya upatikanaji maji safi na salama nchini.

Mkurugenzi Huduma za Ubora wa Maji katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Nadhifa Kemikimba aliyasema hayo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Tanzania na Korea uliokuwa ukijadili teknolojia hiyo ya kutibu maji.


“Suala la maji safi na salama ni hitaji la msingi kwa kila mwananchi, kwa hiyo inapotokea teknolojia tunayoweza kuitumia kurahisisha upatikanaji wa maji safi na salama serikali inakuwa tayari kushirikiana na yeyote au taasisi yoyote inayoleta teknolojia hiyo,” alieleza.

Aidha, alisema upatikanaji wa maji safi na salama kwa sasa kwa mjini hakuna changamoto kubwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliopo lakini kwa upande wa vijijini bado kuna changamoto ingawa serikali inajitahidi kufikia malengo yake.

“Upatikanaji wa maji safi na salama mjini hasa kwa upande wa Dar es salaam ni asilimia 72 na kwa vijijini ni asilimia 50-65 na tunajitahidi ili ifikapo 2020 kwa vijijini tuwe na maji safi na salama kwa asilimia 85 na kwa mjini asilimia 95 na mikakati ipo mingi naamini tutafanikiwa” alisema.

Awali, Balozi wa Korea nchini, Song Geum-Young alisema uhaba wa maji safi na salama ni changamoto kubwa nchini hasa vijijini licha ya kuwa kuna vyanzo vikubwa vya maji kama vile maziwa na mito.

Alisema tayari ameshatembelea kwenye baadhi ya mikoa na miji mbalimbali nchini na kujionea jinsi tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama lilivyokithiri.

Aliongeza kuwa wanatarajia kuanza ujenzi wa mradi wa kusambaza maji mkoani Dodoma na wameshaanza ujenzi wa mradi wa uhifadhi wa maji taka jijini Dar es Salaam imbayo ikikamilika itakuwa ni msaada mkubwa kwa Watanzania.

Kwa upande wake, Rais wa ‎O2 & B Co Limited, SeungHyun Bahn alisema lengo la mkutano huo ni kujadili namna ya kuboresha na kuendeleza upatikanaji wa maji safi na salama kupitia miradi ya kusafisha, kutibu na kuhifadhi maji yatokayo kwenye vyanzo kabla ya kusambazwa kwa matumizi majumbani.
chanzo:Habarileo.

Comments