Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania ni nchi ya kwanza ndani ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya vizuri kiuchumi huku katika ukanda
wa nchi za Jangwa la Sahara ni miongoni mwa nchi tatu zikiwemo Rwanda na
Ethiopia zinazofanya vizuri kiuchumi.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia kwa nchi za
Tanzania, Somalia, Burundi na Malawi, Bella Bird jijini Dar es Salaam
jana wakati ripoti hiyo ilipowasilishwa mbele ya wadau mbalimbali wa
uchumi nchini.
Alisema pamoja na kwamba katika kipindi cha mwaka jana nchi nyingi za
Afrika, zikiwemo za kusini mwa Jangwa la Sahara zilikabiliwa na kushuka
kwa kasi kwa uchumi kunakokadiriwa kuwa ni kwa asilimia 1.5, Tanzania
imeendelea kuonesha ustahimilivu wa kiuchumi katika kipindi chote hicho.
“Viwango vya ukuaji wa uchumi Tanzania vinaendelea kuzipiku nchi za
jirani za Afrika Mashariki. Ustahimilivu huu unatokana na sifa kadhaa za
uchumi wa Tanzania,” alifafanua.
Alisema kwa mujibu wa ripoti hiyo inaonesha uchumi wa Tanzania
kuanzia mwaka 2011 ulikuwa kwa asilimia 7.9, mwaka 2012 asilimia tano,
2013 asilimia saba, 2014 asilimia 6.7, 2015 asilimia 6.7 na mwaka jana
asilimia saba.
Aidha ripoti hiyo kwa upande wa Kenya ilionesha mwaka 2011 uchumi
wake ulikua kwa asilimia sita, 2012 asilimia 4.7, 2013 asilimia 5.5,
2014 asilimia 5.2, 2015 asilimia 6.8 na mwaka jana asilimia 6.8 wakati
Uganda mwaka 2011 ulikuwa kwa asilimia 6.8, 2012 asilimia 3.9, 2013
asilimia nne, 2014 asilimia 5.2, 2015 asilimia 6.5 na mwaka jana
asilimia 4.9.
Alisema Tanzania ina vyanzo anuai vya ukuaji ambapo takribani robo ya
pato lake ghafi la taifa linatokana na kilimo na nusu nyingine
inatokana na sekta tano ambazo ni biashara ya jumla na rejareja, ujenzi,
uzalishaji, viwanda, uchukuzi na utawala wa umma.
“Hali ya uchumi wa Tanzania iko imara lakini hakuna nafasi ya
kubweteka kwani imedhamiria kuendeleza viwango vya sasa vya ukuaji vya
takribani asilimia saba na kufikia asilimia 10 kama ilivyo lengo la
serikali ifikapo mwaka 2020/21 katika kipindi hiki ambacho nchi
inaelekea kwenye uchumi wa viwanda,” alisema.
Alisema nchi hiyo imefanya vizuri kwa kuendelea kuwa na sera makini
za uchumi mkuu ambapo mwaka jana shilingi ya Tanzania ilikuwa imara
kutokana na kuwepo kwa akiba ya kutosha huku mfumuko wa bei ukibaki
katika kiwango cha chini ya wastani ambacho ni asilimia 5.5
ikilinganishwa na mwaka 2015.
Bird alisema kwa upande wa fedha, serikali ya Tanzania inastahili
pongezi kwa kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani hadi kufikia asilimia
14.5 ya pato ghafi la taifa kupitia jitihada za kupunguza misamaha ya
kodi na kudhibiti rushwa.
“Kwa kweli uongozi wa Tanzania unahitaji pongezi kwa hili, lakini
changamoto zimeonekana katika kugharamia bajeti ya maendeleo na mzigo wa
madeni umeshughulikiwa kwa sehemu ndogo, hali iliyoleta athari kwa
wawekezaji kukosa imani lakini pia sekta binafsi kutoshirikishwa vyema,”
alifafanua.
Hata hivyo, alitaja sekta ambazo ikilinganishwa na mwaka 2015, mwaka
jana na mwaka huu zinaendelea kukua nchini humo kuwa ni sekta ya ujenzi
kwa asilimia 18, madini na uchimbaji mawe asilimia 16.5, usafirishaji na
uhifadhi asilimia 17, habari na mawasiliano asilimia 14 na fedha na
bima asilimia 12.
Alitaja sababu zingine za nchi hiyo kufanya vizuri kiuchumi kuwa ni
tangu Rais John Magufuli aingie madarakani mwaka 2015, aliingia na sera
kali iliyolenga kuimarisha utawala wa umma, kudhibiti rushwa na
kuimarisha usimamizi wa kodi hali iliyosaidia kuiongezea mapato ya ndani
nchi hiyo.
Alipongeza juu ya hatua iliyofikiwa ya kuhakikisha huduma ya
upatikanaji wa fedha kwa wote inafikiwa ambapo kwa sasa kutokana na
matumizi ya huduma za kibenki kwa njia ya simu zimewezesha idadi kubwa
ya watanzania kufikiwa na huduma ya fedha tofauti na miaka ya nyuma.
Alisema mwaka 2006 kulikuwa na asilimia 11 tu ya watu wazima
wanaotumia simu za mkononi lakini tangu kuanza kutumika kwa huduma za
kibenki kwa njia ya simu mwaka 2008 kwa sasa jumla ya asilimia 62 ya
watanzania wana akaunti za benki kupitia kampuni za simu kwa
kushirikiana na taasisi za fedha.
Aidha, alisema uchumi huo umeendelea kuimarika ingawa kumekuwepo kwa
changamoto za kudhibiti matumizi ya fedha ambayo kwa namna moja yamekuwa
yakiikandamiza sekta binafsi inayotegemea zaidi serikali kama mteja
wake mkuu.
Alitaja mafanikio na maeneo ambayo matumizi ya fedha yamebanwa kuwa
ni pamoja na uamuzi wa Dk Magufuli kuzuia matumizi yasiyo ya lazima
ikiwemo safari za nje ya nchi, kupunguza malipo yasio ya lazima ya
posho, kufichua watumishi hewa kwenye sekta ya umma ambao takribani
15,000 walibainika na kupiga marufuku mikutano kufanyikia kwenye
mahoteli.
Alitaja changamoto nyingine zinazoikabili sekta ya uchumi kuwa ni
kuendelea kuwepo kwa tatizo la ajira ambapo kwa sasa inakadiriwa kuwepo
kwa vijana 800,000 wanaoingia kwenye soko la ajira kila siku.
chanzo:Habarileo.
Comments