Rais Dkt. Shein amevitaka vyombo vya habari kutoa matukio na maendeleo ya Serikali ili jamii iendelee kujenga imani na Serikali yao.

Dk. Shein ameyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Baraza la Zamani
la Wawakilishi wakati akifungua Semina ya siku moja ya Viongozi,
Watendaji Wakuu wa SMZ, Waandishi wa Habari, Wapiga Picha na Wahariri wa
Vyombo vya Habari vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika hotuba yake ya ufunguzi huo, Dk. Shein alisema kuwa ni muhimu
kwa waandishi wa habari wa vyombo vya umma kuvifahamu vyema vipaumbele
vya serikali na masuala ambayo kwa wakati huu Serikali imeyatekeleza
vizuri na kuwataka viongozi wa taasisi husika kushirikiana na waandishi
wa habari wa vyombo vya umma kutangaza mafanikio hayo.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa historia ya vyombo vya habari vya
Zanzibar na kusema kuwa Zanzibar ina historia ndefu ya vyombo vya
habari ambapo Sauti ya Tanzania ya Zanzibar ilikuwa ya mwanzo kuanzishwa
Afrika kwenye miaka ya 50 na ya mwanzo kuanzisha Televisheni ya rangi
katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Pia, Shein alieleza kuridhika kwake na mabadiliko makubwa
yanayoendelea kufanywa hivi sasa katika Shirika la Habari la Utangazaji
Zanzibar (ZBC) Radio na TV, pamoja na Gazeti la Zanzibar Leo ili
kuhakikisha vyombo hivyo vinakwenda sambamba na sayansi na teknolojia.
Aidha, Dk. Shein aliwataka viongozi wa Serikali na Waandishi wa
habari kujenga utamaduni wa kuweka kumbukumbu za matukio na ahadi za
Serikali ili kuweza kufuatilia na kufahamu hatua za utekelezaji wa ahadi
hizo na kwa wakati muwafaka kuiarifu jamii hali halisi.
Alieleza kuwa hatua hiyo itaondosha uwezekano wa watu wasioyayajua
mambo hayo kueneza habari zisizokuwa za kweli “Siku hizi tumbaku
zimekuwa nyingi na ili tumbaku zisitokezee ni jukumu la viongozi wa
Serikali kutoa taarifa sahihi na wakati sahihi katika vyombo vya
habari”,alisema Dk. Shein.
Dk. Shein alisema kuwa vyombo vya habari vina umuhimu wa pekee katika
kusukuma mbele maendeleo ya nchi na kukuza demokrasia, hivyo ni lazima
ifahamike kwamba inapodhamiriwa kuleta maendeleo endelevu na kujenga
demokrasia ya kweli ni lazima iwepo jamii yenye uwelewa wa mambo ya
ndani na nje ya nchi.
Alisisitiza kuwa ni jukumu la Serikali kuwapa wananchi taarifa kila
inapobidi kupitia vyombo vya habari na ndipo kutokana na umuhimu huo
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania zimetambua umuhimu huo kwenye Katiba zake ambapo kwa upande wa
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Sura ya tatu, kifungu cha 18(2).
Aliongeza kuwa vyombo vya habari vya Serikali vinapaswa kujenga
taswira kwa umma kutokana na taarifa zake inazozitoa na vyombo binafsi
na si mbadala wa vyombo vya Serikali bali vina kazi ya kuongeza nguvu
kwa vyombo hivyo.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa vyombo vya Habari vya binafsi vina kazi
ya kushirikiana pamoja na vyombo vya habari vya Serikali na si kuipinga
Serikali kwani lengo ni kuwatumikia wananchi.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwataka viongozi wote wa Serikali kutoa
taarifa kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa mipango na mikakati ya
Serikali kwenye vyombo vya habari na kutowaogopa waandishi wa habari au
kuogopa maswali yao.
Dk. Shein alieleza matumaini yake kuwa baada ya semina hiyo ukurasa
mpya wa maendeleo utafunguliwa katika utoaji wa taarifa kwa wananchi
kupitia vyombo vya habari vya Serikali na hata vile vya binafsi.
Katika maelezo yake Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa
waandishi wa Habari wa vyombo vya Habari vya Serikali na vile vya
binafsi kwa kazi nzuri wanazofanya za kutoa habari.
Nae Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Rashid Ali Juma
alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kuwa na wazo zuri la kufanyika kwa
Semina hiyo ambayo ni muhimu kwa viongozi na waandishi wa Habari kwa
maendeleo ya nchi.
Aliongeza kuwa Semina hiyo italeta mashirikiano makubwa hatua ambayo
itawasaidia wananchi kuendelea kupata habari kutoka vyombo vya habari
vya Serikali na vile vya binafsi.
Mapema, Katibu Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi
Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisema kuwa Semina hiyo ya siku moja ina
madhumuni ya kujenga maelewano na mahusiano mazuri kati ya waandishi wa
habari na viongozi ambao ni watunga Sera pamoja na kuelewa wajibu na
majukumu ya viongozi na waandishi wa habari hasa wa vyombo vya umma.
Katika semina hiyo Mada ya Umuhimu wa Vyombo vya Habari na Maendeleo
ya Taifa ilitolewa na Hassan Abdallah Mitawi ambaye ni Naibu Katibu Mkuu
Habari, katika Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo na baadae
michango mbali mbali ilitolewa.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
chanzo:zanzibar24.
Comments