MFANYABIASHARA wa kuku, Michael Gadi (52) amedai kuwa baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ngulu Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro walimsingizia kesi ya mauaji baada ya kushindwa kumfukuza kwa kuhofia atawaambukiza Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Mtuhumiwa huyo wa mauwaji alieleza hayo juzi mbele ya Jaji Patricia Fikirini wakati akijitetea dhidi ya mashitaka ya mauaji ya bila kukusudia yanayomkabili katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi.
Wakati akijitetea, Gadi alidai kuwa Mei 18, 2014, alitoka Same na kurudi nyumbani saa 10 jioni, akapumzika ilipofika usiku alisikia kelele, akafungua dirisha na kuona watu wengi pamoja na askari wa mgambo wakimtaka afungue mlango lakini alikataa kufanya hivyo hadi balozi atakapofika. Aliendelea kudai baada ya balozi kufika alifungua mlango na askari walimkamata na kukagua ndani kwake, wakachukua kisu na kumpeleka katika kituo kidogo cha polisi cha Ngulu na baadaye alihamishiwa kituo cha Mwanga.
Gadi alidai baada ya siku tatu walimtoa kituoni na kumueleza wanakwenda nyumbani kwake kukagua tena, walipofika akawaambia hawezi kufungua mlango kwa sababu askari anayeitwa Samweli alichukua ufunguo wa nyumbani kwake. Alidai walimtafuta askari Samweli akawafungulia mlango “wakati wakiendelea kukagua nilisikia wakisema kisu hiki hapa kwenye godoro, wakaniuliza hiki kisu cha nani? nikawaambia siyo changu wamuulize aliyekuwa na ufunguo wa chumba changu”.
Katika ushahidi wake Gadi alikana maelezo aliyoyatoa kituo cha polisi pia alidai hajawahi kuzungumza na Masanga (marehemu) zaidi ya kujua jina lake. Baada ya kusikiliza ushahidi huo, Jaji Fikirini aliahirisha kesi hiyo hadi leo kwa ajili ya pande zote mbili kuwasilisha majumuisho ya hoja, upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi saba na mshitakiwa alijitetea mwenyewe.
chanzo:zanzibar24.
Comments