Mgogoro
ulioanza kufukuta kwenye mitandao ya kijamii kati ya mmiliki wa
makampuni ya Global Publishers, Erick Shigongo na meneja wa Diamond
Platinumz, Babu Tale umechukua sura mpya baada ya meneja huyo kudai
ametishiwa.
Mtafaruku
kati ya wawili hao ulianza baada ya Shigongo kuandika katika ukurasa
wake wa Instagram ushauri wake kwa Diamond akidai kuwa kitendo cha
kujikita katika matamasha ya kimataifa na kuyaweka kando ya ndani huku
akitaka kulipwa zaidi ya shilingi milioni 100 pia ndani ya nchi
kutamgharimu hususan kupoteza mashabiki wa ndani siku za usoni.
Akifunguka
jana kupitia ‘Shilawadu’ ya Clouds TV, Babu Tale ambaye alimtaja
Shigongo kuwa ni mtani wake kikabila, alimlalamikia kwa kudai kuwa
alimpigia simu na kumweleza maneno ambayo aliyatafsiri kama vitisho.
Alidai
kuwa baada ya kumpigia simu na mwandishi huyo nguli wa vitabu vya
uhamasishaji wa kiuchumi na masimulizi alimuuliza ‘kama anataka vita’
kati yao baada ya maelezo.
“Nikipata
matatizo leo, ina maana aliyeniambia ‘ninataka vita’ ina maana
amenisababishia matatizo. Lakini sitaishia hapa nitafuata vyombo vya
sheria ili vinilinde,” alisema Babu Tale.
Meneja
huyo wa WCB alionesha kushangazwa na kitendo cha Shigongo kumshauri
Diamond kupitia Instagram, akidai kuwa kama angekuwa na nia njema kweli
angemuita na kumshauri hata akiwa ofisini kwake.
Tale
alienda mbali na kueleza kuwa Shigongo anampango wa kumuangusha katika
biashara zake baada ya wawili hao kushindwana katika mambo yao ya
kibiashara. Alimlaumu Shigongo pia kwa kuweka hadharani ujumbe
aliomtumia kwenye simu.
Bado
haijajulikana uhalisia wa chanzo cha mgogoro huo, lakini dalili zote
zinaonesha huenda kukawa na msuguano wa kibiashara au kutoelewana katika
hoja dhidi ya Diamond Platinumz ambaye ni bidhaa kubwa Afrika iliyo
kwenye mikono ya Babu Tale na Salaam.
CHANZO:MPEKUZIBLOG.
Comments