Hali hiyo iliibuka baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge
kumwita Lissu kuwasilisha hotuba yake. Kabla ya kuanza kusoma, Jenista
ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Serikali alimuomba Mwenyekiti kuizuia
hotuba hiyo kwa kuwa imejaa maneno ambayo masuala yake yapo mahakamani
na pia amezungumzia mwenendo wa Rais, jambo ambalo ni kinyume cha Kanuni
za Bunge.
Alisema hotuba hiyo ina mambo mengi yanayokiuka kanuni. Alisema
katika hotuba hiyo kuna mambo ya mienendo ya kesi ambazo zipo
mahakamani, jambo ambalo ni kinyume na kanuni na pia, kuna mambo
yanayozungumzia mwenendo wa Rais, jambo ambalo ni kinyume cha Kanuni
Kifungu 64 (1) (e).
“Naomba nitoe utaratibu ni kwanini hoja hii
irudishwe mezani kwako na maeneo yanayokiuka kanuni hizi yaweze
kuondolewa na ndipo iweze kuwasilishwa ndani ya Bunge hili,” alisema
Waziri Mhagama.
Hata hivyo, Chenge alimruhusu Lissu kusoma hotuba yake huku akimtaka
Waziri Mhagama kuainisha maeneo yaliyokuwa na maneno yenye ukakasi.
Wakati huo Lissu alianza kusoma hotuba yake, lakini Chenge alimkatisha
na kumtaka kuyafuta maneno hayo, kwa kuwa hayapo kwenye hotuba yake na
kumtaka kwenda moja kwa moja kwenye hotuba.
Akisoma hotuba hiyo, Lissu alisema hiyo ni mara yake ya saba kusimama
mbele ya Bunge kutoa maoni ya kambi rasmi ya upinzani kuhusu Wizara ya
Mambo ya Katiba na Sheria na ameshangaa kuona Wizara hiyo imekuwa
ikiongoza kwa kuwa na mabadiliko mengi ya mawaziri kuliko wizara
nyingine.
Alisema baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010, alianza Celina
Kombani (sasa marehemu) kisha wakafuata Mathias Chakawe, Dk Asha-Rose
Migiro, Dk Harrison Mwanyembe na sasa Profesa Palamagamba Kabudi.
Alisema ingawa Profesa Kabudi anaweza kuwa mgeni bungeni, lakini si
katika uelewa wa matatizo makubwa ya kisiasa na kikatiba nchini.
Alimkumbusha majukumu makubwa na mazito anayolazimika kuyabeba kwa
nafasi yake hiyo.
chanzo:Habarileo.
Comments