Alitoa maagizo hayo hivi karibuni katika Kijiji cha Negezi wilayani
Kishapu wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme
Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kwa mkoa huo.
“Tumia wataalamu/vibarua vijana kutoka maeneo haya. Hatutapenda
uajiri watu kutoka mbali wakati wafanyakazi wenye sifa wako hapa hapa,”
alisema Dk Kalemani na kumwagiza mkandarasi huyo kuhakikisha anawalipa
vibarua mara moja kila wanapokamilisha kazi husika. “Hakuna kulaza
malipo kwa sababu sisi tunakulipa vizuri,” alieleza.
Sambamba na maagizo hayo, Dk Kalemani aliutaka uongozi wa Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani humo kujipanga na kumsimamia mkandarasi
husika ili kuhakikisha anafanya kazi saa 24 kwa siku.
Alisisitiza kuwa ofisa yeyote atakayelegalega kumsimamia mkandarasi
husika kadri inavyotakiwa atawajibishwa kwa kuondolewa katika nafasi
yake.
Naibu Waziri pia aliwaelekeza Tanesco kuhakikisha wanawafuata wateja
na kuwapatia huduma mahala walipo badala ya kusubiri wateja wawafuate
katika ofisi zao, ambazo ni chache na ziko mbali na makazi ya wananchi
wengi hususan walioko vijijini.
Kutokana na maelekezo hayo; aliuomba uongozi wa halmashauri
mbalimbali za Mkoa wa Shinyanga, kuanzisha vit uo maalumu ambavyo
vitatumiwa na maofisa wa Tanesco kuwahudumia wateja walioko katika
maeneo yao.
chanzo:habarileo.
Comments