
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar
Dkt. Abdallah Juma Abdallah “Mabod” wakati akizungumzia historia ya
maisha ya Mwasisi wa ASP ambayo ni CCM kwa sasa Marehemu Mzee Karume
huko Afisini kwake Kisiwandui Unguja.
Amesema Mwasisi huyo alikuwa ni kiongozi anayepinga utengano na
ubaguzi misingi ya kidini, kikabila na kisiasa ndio maana katika Baraza
la mwanzo la Mawaziri kupitia Baraza la Wawakilishi la Wakati huo
aliteuwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani ili kujenga Umoja wa
kitaifa na kuondosha ubaguzi.
Aidha alisema kuwa viongozi walioteuliwa kutoka vyama vya upinzani
walikuwa ni waadilifu waliofuata miongozo na matakwa ya serikali kwa
wakati huo licha ya kujitokeza kwa vitendo vya usaliti kwa viongozi hao.
“ Mzee karume alikuwa na moyo wa huruma na akiwapenda wananchi wa
visiwa vya Zanzibar wawe na maendeleo endelevu.”, alisema Dkt. Mabodi.
Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa lengo la kufanyika kwa Mapinduzi
ya Mwaka 1964, lilikuwa ni kurejesha heshima ya wazawa waliotawaliwa
kimabavu na utawala wa Kisultani kwa zaidi ya miaka 100.
Alisema baada ya mapinduzi hayo Marehemu Mzee Karume na Jopo lake la
Umoja wa Vijana wa ASP, waliweka mipango mikakati ya kuimarisha
maendeleo ya Zanzibar.
Pia aliweka vipaumbe mbali mbali vikiwemo kuanziasha mpango wa
kuboresha Sekta ya Elimu na Afya kwa kuwapeleka vijana mbali mbali nje
ya nchi ikiwemo China, Urusi, Cuba na mataifa mengine ili wapate utalamu
wa fani tofauti zikiwemo Udaktari na masuala ya Uongozi ili
kuharakisha maendeleo ya nchi.
Hata hivyo aliweka mfumo wa Elimu bure ili Watoto wa Kiafrika
waliokuwa hawana fursa ya kusoma wakati huo wajifunze na kuelimika ili
waweze kusaidia katika masuala mbali mbali ya kiutendaji.
Dkt. Mabodi alisema kuwa Mzee Karume alikuwa ni kiongozi jasiri na
asiyetaka kukaa Ofisini bali alikuwa akitembea maeneo mbali mbali na
kujionea mwenyewe changamoto zinazowakabili wananchi, tofauti na baadhi
ya viongozi wa sasa wanaosubiri taarifa za utekelezaji ofisini.
Hata hivyo alisema Mzee Abeid Amani katika Harakati za kupinga
ubaguzi ambao ulikuwa umejenga ngome, enzi za utawala wa kifalme
aliwatangazia wananchi kuwa wanatakiwa kuoana makabila mbali mbali ili
kuchanganya rangi kwa lengo la kufuta ubaguzi uliokuwa kukisambazwa na
watu waliokuwa ni miongoni mwa Waliopinduliwa.
Aidha alisema Mzee Karume pamoja na mambo mema aliyoyafanya enzi za
uhai wake pia ni mwasisi wa kwanza wa Demokrasia kwani aliwakaribisha
mataifa mbali mbali kuja Zanzibar kuwekeza na kushauri masuala ya
Kisiasa.
Aliimarisha miundombinu ya barabara na kujenga nyumba za kisasa
ambazo hivi sasa zinajulikana kama nyumba za maendeleo Unguja na Pemba.
Pia aliimarisha Sekta ya Mawasiliano kwa kuanzisha Televisheni ya
mwanzo ya rangi Afrika Mashariki na kati iliyoitwa TVZ ambayo kwa sasa
ni ZBC TV, sambamba na radio ya kisasa ya Sauti ya Tanzania Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu huyo aliweka wazi kuwa kiongozi huyo ametenda mengi
mazuri kwa nchi ya Zanzibar, hivyo viongozi na watendaji wa sasa
waendeleze mambo mema yaliyoachwa huku nao wakibuni vitu vingine vipya
vinavyoendana na wakati uliopo sasa.
Pia alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi
Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kufanyia kazi kwa vitendo kauli mbiu ya “
Zanzibar kujitawala yenyewe kielimu, kiafya na kimiundombinu ya kisasa”
huku ikipiga vita adui ujinga na maradhi.
Pamoja na hayo alimpongeza pia Rais wa Jamhuri ya muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa msimamo wake wa kulinda Muungano
wa Serikali mbili na Mapinduzi ya Zanzibar mambo ambyo ndio urithi wa
Waasisi wa ASP na TANU wakiwemo Marehemu Mzee Karume na Hayati Mwl.
Nyerere.
Pamoja na hayo aliwambia wananchi kuwa kila ifikapo April 7 ya kila
mwaka ni maadhimisho ya kumbukumbu ya siku ya mashujaa wa Zanzibar na
waasisi wote waliofariki , na sio sherehe ndio maana panafanyika hitima
na kuombwa dua kwa lengo la kuenzi juhudi zao.
Na: IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
chanzo: zanzibar24.
Comments