
Walisema wachumaji wakubwa wa zao la karafuu ni watoto wenye umri
kati ya miaka 14 hadi 17, hivyo ni vyema kwenye marekebisho ya sheria ya
fidia, watoto wenye umri huo nao wakatambuliwa na sheria ili kulipwa
fidia.
Wananchi hao walieleza hayo mbele ya Tume ya Kurekebisha Sheria,
inayoongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mshibe Ali Bakari, wakati
ilipokutana na wananchi hao, ili kukusanya maoni yao, juu ya kuzifanyia
mapitio sheria za usalama kazini na ile ya fidia zote za mwaka 2005.
Maoni ya wananchi hao, yalikuja kufutia sheria ya sasa ya fidia ya
mwaka 2005 kwamba, haimtambui kifidia kwa mtu alienguka wakati akichuma
karafuu, kama hajafikia umri wa miaka 18.
Mjumbe wa mkutano huo Juma Bakar Shoka, alisema wachumaji hasa wa zao
la karafuu ni watoto wenye umri kuanzia miaka 14 na kuendelea, hivyo
lazima sheria iwatambue kulipwa fidia.
“Mimi napendekeza kwenye sheria mpya ijayo ya fidia, na hawa watoto
walipwe fidia, maana ndio hasa wenyewe wanaozichuma karafuu na hata
skuli wakati mwengine hufungwa’’,alipendekeza.
Nae Salum Omar alisema watu wenye umri mkubwa, wengi wao sio
wachumaji hasa wa zao taifa la karafuu, na badala yake watoto wenye umri
wa kati, ndio wahusika wakuu.
“Hata mimi napendekeza sheria ya fidia ijayo, iwatambue watoto wenye
umri kuanzia umri wa miaka 14 na kuendelea, maana tukifanya kinyume
chake, tutawakosesha haki yao ya kujifunza kuchuma karafuu’’,alisema.
Kwa upande wake Rashid Abdalla, alisema hata sheria inayokuja
ielekeze wapi fedha hizo zinapatikana na kusiwe na urasimu, na kumfanya
mpatwa na ajali kujuta kuzifuatilia.
Akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria
Zanzibar Jaji Mshibe Ali Bakar, alisema ingawa sheria za kimataifa
zinakataza mtoto kufanyishwa kazi zenye kuhatarisha maisha yake, lakini
hilo wataliangalia kwa ukaribu.
Katika hatua nyengine Mwenyekiti huyo, alisema lengo la kuzifanyia
marekebisho sheria za fidia na ile ya usalama kazini za mwaka 2005,
kuhakikisha wananchi wote wanaishi kwa usawa.
Sheria ambazo Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar inazifanyia mapitio
ni ile sheria ya fidia ya kazini no 15 ya mwaka 1986 pamoja na
marekebisho yake ya mwaka 2005 na sheria ya usalama kazini no 8 ya mwaka
2005.
chanzo:zanzibar24.
Comments