Ukame na njaa vyaendelea kuua watu barani Afrika.

Wimbi la vifo vinavyotokana na ukame na njaa limezikumba nchi kadhaa za Afrika hususan mashariki mwa bara hilo.

Ripoti zinasema kuwa watu wasiopungua 110 wamefariki dunia kutokana na njaa nchini Somalia. Waziri Mkuu wa Somalia, Ali Khaire ametangaza kuwa, njaa iliyolikumba eneo la Bay huko kusini magharibi imeua watu wasiopungua 110 katika kipindi cha masaa 48 yaliyopita. 

Hizo zilikuwa takwimu rasmi za kwanza kutolewa na serikali ya Somalia kuhusu idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na ukame ulioikumba nchi hiyo. 
Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa, watu milioni tano wanahitaji misaada ya dharura ya chakula nchini Somalia kutokana na ukame mkubwa ulioiathiri nchi hiyo. 
Kutokana na hali hiyo Rais wa Somalia ameomba msaada wa kimataifa wa kukabiliana na ukame na njaa nchini humo. Rais Mohamed Abdullahi Farmajo ametangaza janga la njaa lililoikumba nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kuwa ni maafa ya taifa. 
Shirika la Afya Duniani (WHO) pia limetahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea maafa makubwa nchini Somalia kama yale wa mwaka 2011 ambayo yalisababisha vifo vya malaki ya watu.
Wimbi la ukame limeyakumba maeneo kadhaa ya Afrika kwa miaka kadhaa mtawalia. Hali hiyo imesababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na gesi za sumu na viwandani (greenhouse gases). 
Ukame na mafuriko ya mara kwa mara katika nchi nyingi za Afrika yameharibu mazao na ardhi za kilimo na kuwalazimisha mamilioni ya watu kuhama makazi na mashamba yao na kuwa wakimbizi. 
Takwimu na ripoti za mashirika ya kimataifa zinaonesha kuwa, zaidi ya watu milioni 40 katika nchi nyingi za Afrika wameathiriwa na njaa na ukame uliosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa kama El Nino. 
Hii ni pamoja na kuwa, nchi za Afrika zimeendelea kuwa wahanga wa gesi za sumu zinazozalishwa kwa wingi na nchi kubwa na zilizoendelea za Magharibi. 
Vilevile miundombinu dhaifu, utumiaji mbaya wa vyanzo vya maji, jamii kubwa ya watu, kutokuwa na teknolojia ya kisasa, vita vya wenyewe kwa wenyewe na utumiaji wa mbinu za zamani za kilimo vinatajwa kuwa ni miongoni mwa mambo yanayochangia katika mgogoro wa njaa katika nchi nyingi za bara la Afrika.
Kwa muda sasa jumuiya za kimataifa zimetahadharisha kuwa, nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na hatari ya ukame na njaa. 
Ripoi za Umoja wa Mataifa zinasema watu zaidi ya milioni 20 barani humo wanaishi katika hali ilisiyo ya kuridhisha na wanakabiliwa na hatari ya baa la njaa. 
Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa, jumuiya hizo za kimataifa zimetosheka tu kwa kutoa tahadhari bila ya kuchukua hatua za maana za kivitendo za kuwasaidia Waafrika wanaotishiwa na baa la njaa. 
Nchi nyingi za Magharibi pia zinalaumiwa kwa kutotoa michango ya uanachama wao katika jumuiya za kimataifa, suala ambalo linatatiza juhudi za kupambana na baa la njaa huko Afrika.
Kwa vyovyote vile hali ya sasa katika baadhi ya nchi za Afrika inailazimu jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kwa ajili ya kuokoa maisha ya mamilioni ya wanadamu wanaokabiliwa na hatari ya kifo kutokana na ukame na njaa hususan katika eneo la Pembe ya Afrika na mashariki mwa bara hilo.   
chanzo:parstoday.

Comments