Tasaf kuzifanyia uhakiki na kuziondoa kaya maskini zilizomaliza muda wake katika Mradi huo.

Mkuu wa kitengo cha habari kutoka katika mradi wa Tasaf Bi. Zuhura Mdungi amesema, mradi wa Tasaf unampango wa kuziondoa kaya Maskini zilizonufaika na kumaliza muda wake baada ya kuzifanyia uhakiki juu ya hatua waliyofikia katika miradi yao iliyo chini ya Tasaf hivyo kuweza kuzipa fursa kaya nyengine ziweze kunufaika na Mradi huo.

Akizungumza baada ya ziara ya kuangalia maendeleo yaliofikiwa na miradi ilioanzishwa na kaya Maskini
kupitia Mradi wa tasaf, Bi. Zuhura Mdungi amesema lengo la kutolewa fedha kwa kaya masikini ni kuwakomboa kimaisha hivyo ni vyema kwa wanao nufaika na fedha hizo kuzitumia katika malengo yaliokusudiwa.
Aidha amesema serikali katika kuendeleza Mradi huo nchini imelenga kuwaondoa wanakaya wote waliomaliza muda na kunufaika na mradi huo ili kuwasajili wanakaya wapya waliokosa fursa katika kipindi kilichopita isipokuwa wale wanaowalea watoto yatima.
Kwa upande wao wanufaika wa mradi wa Tasaf wamesema uwepo wa mradi wa tasaf umewasadia katika kujikwamua kiuchumi licha ya kukabiliwa na matatizo madogo madogo ikiwemo uwepo wa kima kidogo cha malipo wanachopewa na Serikali.
Akielezea mafanikio waliopata Bi Jabu Omar amesema “Maisha yangu yalikuwa ya kimaskini hata nyumba ya kuishi nilikuwa sina, lakini nashukuru kwa mradi wa Tasaf kuweza kunikwamua kiuchumi na kuweza kuendeleza kilimo cha  mananasi pamoja na mihogo, kilimo ambacho kinaniwezesha kusomesha watoto wangu pamoja na kujenga nyumba ya udongo’’.
“Awali nilikuwa naishi katika nyumba ya udongo ambayo haikuwa katika hali nzuri, lakini kwa sasa nimeweza kujenga nyumba ya tofali ya chumba kimoja na ukumbi na kuweza kusomesha watoto wangu bila ya kuwa tegemezi kwa mtu yoyote  naushukuru sana mradi wa tasaf umenisaidia’’Alisema Bi hidaya Mjaka Mkulima wa Mahindi kutoka kaya Masikini.
Hata hivyo Maryam Hussein Mwenyekiti wa Kikundi cha AMANI GROUP kinachojishughulisha na kilimo cha Mihogo Na MbogaMboga alisema “Tunaishukuru serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Zanzibar  kwa kutuandalia Mpango huu ambao unatusaidia kuondokana na umasikini, lakini wito wangu kwao ni kuendelea kutuunga mkono sisi ambao tunajiendeleza na kilimo ili tuweze kufikia kilimo cha Biashara’’.
Miongoni mwa Shughuli wanayojishughulisha kina mama hao ni pamoja na kilimo cha Mahindi, Mananasi, Mihogo na Mbogamboga ili kujipatia kipato cha kuhudumia familia zao.

chanzo: Zanzibar24.

Comments