Serikali yasifu kasi urejeshaji miundombinu mkoani Kagera.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Kagera kwa hatua iliyofikiwa katika kurejesha miundombinu mbalimbali iliyoathiriwa na tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, mwaka jana lililoua watu 17 na kuharibu miundombinu mingi.


Waziri huyo alionesha kuridhishwa kwake baada ya kufanya ziara mkoani humo mapema wiki hii kwa lengo la kutathmini utekelezaji unaoendelea katika kurejea miundombinu ili wananchi waendelee kutumia huduma hizo kama kawaida.

Katika ziara hiyo, Jenista alitembelea Shule ya Sekondari Nyakato, Ihumona na Omumwani, Kituo cha Afya cha Kabyaile-Ishezina na Kituo cha Kulelea Wazee cha Kiilima na kubaini kuwa ujenzi wa kituo kipya cha afya cha Kabyaile-Ishozi kilichofikia asilimia 80, umetumia takribani kiasi cha Sh milioni 381.5.

“Nikiri kwamba ukiacha baadhi ya mapungufu kwa watendaji wachache, wengi mmetupa ushirikiano mzuri kwa kulinganisha hali ilivyokuwa kwa kuangalia tukio lilivyotokea na hadi hatua za kukabili hatimaye kurejesha hali,” alisema Jenista, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi yake.

Alipongeza jinsi wananchi wa mkoa huo walivyoendelea kushirikiana katika kutekeleza majukumu hadi kufikia lengo la kurejesha hali ya kawaida ya mkoa huo katika maeneo yaliyoathirika na tetemeko lililokuwa na ukubwa wa 5.9 katika vipimo vya Ritcher.

“Kama si ushirikiano wa pamoja kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Mkoa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania huenda tusingefika hapa, hivyo tuna kila sababu ya kupongeza juhudi hizi kwa niaba ya serikali hususani Ofisi ya Waziri Mku, tumefarijika kwa ushirikiano wenu,”alisisitiza.

Pamoja na pongezi hizo, Waziri alimtaka Katibu Tawala wa Mkoa huo, Kamishna Diwani Athumani kuendelea kuzingatia taratibu za manunuzi na kila eneo linalofanyiwa kazi kufuata taratibu, za manunuzi zilizopo kwani kwa atakayekiuka sheria na taratibu hakutakuwa na msamaha.
 chanzo:Habarileo.

Comments