Mara baada ya kuwasili jana mchana, Barrow alikutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Macky Sall, katika Ikulu ya Rais mjini Dakar. Duru za habari zinaarifu kuwa, wawili hao wamejadili masuala ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga mbali mbali.
Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Ofisi ya Rais wa Senegal, Hamidou Elhadji Kassé amesema kuwa, leo Ijumaa Rais Barrow atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa kidini.
Aidha Rais huyo wa Gambia na mwenyeji wake Macky Sall wanatazamiwa kushuhudia kusainiwa mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kesho Jumamosi.
Ikumbukwe kuwa, Barrow alikimbilia nchi jirani ya Senegal Januari 15 akihofia usalama wake baada ya mtangulizi wake Yahya Jammeh kukatalia madarakani, na aliapishwa katika ubalozi wa Gambia mjini Dakar Januari 19.
Jammeh aliyeitawala Gambia kwa kipindi cha miaka 22 aliondoka madarakani kutokana na mashinikizo ya kieneo na kimataifa, baada ya hatua yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika Disemba mwaka jana, ambayo awali aliyakubali.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS ilituma vikosi vya kieneo kwenda kumshinikiza Jammeh kuachia ngazi.
chanzo;parstoday.
Comments