Marekani yakiri kuwaua raia 12 Yemen

Kamanda wa ngazi za juu Marekani amekiri kuwa raia 12 waliuawa mwishoni mwa mwezi Januari nchini Yemen wakati jeshi la Marekani liliposhambulia eneo lililodaiwa kuwa ngome ya magaidi wa Al Qaeda nchini Yemen.

Mkuu wa Kamandi Kuu ya Marekani Jenerali Joseph Votel ameiambia Kamati ya Ulinzi katika Bunge la Senate kuwa raia baina ya wanne na 12 waliuawa katika hujuma ya kijeshi katika mkoa wa Al Bayda katikati mwa Yemen.

Aidha amekiri kuwa Marekani ilipata hasara katika oparesheni hiyo ya mwezi Januari kwani ndege yake aina ya MV-22 Osprey iliharibiwa ambapo inadaiwa kuwa magaidi 14 wa al Qaeda pia waliuawa.
Hayo yanajiri wakati Saudia, kwa kushirikiana na Marekani, ilianzisha hujuma za kila upande dhidi ya Yemen tarehe 26 Machi mwaka 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani kibaraka wake Abdrabbuh Mansur Hadi rais wa zamani wa Yemen ambaye alijiuzulu nafasi hiyo na kukimbilia Saudia. Hadi sasa watu takribani 12,000 wameuawa katika hujuma hiyo.
Marekani imekuwa ikitumia ndege zake zisizo na rubani kuhujumu watu inaowadhania kuwa ni magaidi katika nchi kama Somalia, Pakistan, Afghanistan na Yemen. Hata hivyo mashahidi wanasema aghalabu ya wanaopoteza maisha katika hujuma hizo ni raia wa kawaida wasio na hatia.
Umoja wa Mataifa unailaumu Marekani kwa mauaji yanayofanywa na ndege zake zisizo na rubani katika nchi mbalimbali ukisema kuwa yanakiuka sheria za kimataifa.
chanzo:parstoday.

Comments