Nape aliunda timu hiyo ya watu watano juzi ikiongozwa na Mkurugenzi
wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Hassan Abbas, na aliipa muda wa saa 24
hadi jana iwe imekamilisha kazi yake.
Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni, timu hiyo ilikuwa
haijawasilisha taarifa yake kwa waziri huyo na hakukuwa na taarifa rasmi
kuhusu kutowasilishwa kwa taarifa hiyo.
Lakini jana mchana, katikaakaunti yake ya Tweeter, Waziri Nape
aliandika: “Kuna simu nyingi juu ya ripoti. Nawaomba tutulie Kamati
wanamaliza kazi yao, ikikamilika tutaarifiwa muda na mahali
nitakapokabidhiwa.”
Akizungumza Dar es Salaam juzi baada ya kutembelea Clouds Media
Group, Mikocheni, Nape alisema kama serikali, kilichotokea ni kitendo
ambacho kimewashtua wengi na hata dunia kwa ujumla kwa kuwa hata katika
historia haijawahi kutokea suala kama hilo.
Alisema kutokana na kilichotokea, ameunda timu ya watu watano
wakifanya kazi kwa saa 24 ili kujua na upande wa pili ambao ni wa
Makonda unazungumziaje suala hilo na baadaye watamkabidhi ripoti ambayo
ataitoa leo saa 8:00 mchana.
Aliwataja wanaounda timu hiyo itakayoongozwa na Mkurugenzi wa Idara
ya Habari (Maelezo), Dk Abbas Hassan, ni Mwakilishi kutoka Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mabel Masasi, Mhariri Mwandamizi kutoka
Kampuni ya The Guardian, Jesse Kwayu, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ambaye pia ni Mkurugenzi wa
Kampuni ya Jamhuri na Mhariri wa Wapo Radio, Neng’ida Johannes.
Waziri Nape alisema serikali imesikitishwa na jambo hilo, lakini
lazima kutenda haki kwa kumsikiliza pia mkuu wa mkoa na watu wake ili
kujiridhisha halafu ndipo hatua nyingine zitakapoweza kuchukuliwa.
Naye Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge
Mutahaba alilezea namna Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
alivyovamia ofisi za chombo hicho cha habari akiambatana na askari
waliobeba silaha.
Akizungumza katika mahojiano yaliyofanyika kwenye kipindi
kinachorushwa na kampuni hiyo juzi, Mutahaba alisema wanalaani kitendo
hicho cha Makonda kwa kuwa kimewaacha katika hali mbaya wafanyakazi wa
kampuni hiyo.
Alisema chanzo cha tukio hilo, kilianza tangu Alhamisi iliyopita
wakati uongozi wa kampuni hiyo ulipokuwa kwenye kikao na Kamati ya
Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TRA), ambapo walipata ugeni
wa RC Makonda katika kikao hicho.
“Baada ya hapo wakati kikao kimemalizika nikiwa natoka nikakutana na
vijana wanatangaza katika kipindi cha Shirika la Wambea Duniani
(Shilawadu) kupitia kampuni hiyo, wakiwa wanazungumza na mkuu huyo wa
mkoa,” alisema Mutahaba.
Alisema mmoja wa vijana wale alimfuata na kumueleza juu ya kuwepo kwa
fununu za habari kubwa inayomhusu Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,
Josephat Gwajima, kuzaa na mmoja wa waumini wake, lakini bado fununu
hizo pamoja na kukamilika upande mmoja, hazijathibitishwa upande wa
pili.
“Niliwaambia kuwa kama habari hiyo hata kama ni nzuri vipi kama bado
haina upande wa pili kama maadili ya taaluma ya uandishi wa habari
yanavyotaka kamwe isirushwe hewani. Sikuishia hapo nilimpigia simu mkuu
wa vipindi Carry, nikamuonya asiruhusu habari hiyo iruke hewani kama
haijawa balanced,” alifafanua.
Alisema siku hiyo, majira ya saa 10 jioni alipigiwa simu na Askofu
Gwajima akiulizia taarifa za kuwepo kwa habari inayomhusu inayotarajiwa
kurushwa katika vyombo vya habari vya kampuni hiyo kupitia kipindi cha
Shilawadu.
Alisema alimjibu mtumishi huyo wa Mungu kuwa ni kweli alikuwa na
taarifa za kuwepo kwa habari hiyo, ingawa yeye mwenyewe haifahamu
kiundani na kufafanua kuwa alishaagiza isirushwe hewani mpaka
itakapokamilika kwa upande wa pili kupatikana na baadaye kupata habari
kwamba Makonda amevamia kituo hicho akishinikiza habari hiyo itoke.
chanzo:Habarileo.
Comments