Serikali
ya Kenya imeiomba Tanzania kuiruhusu kuajiri madaktari kutoka nchini
humo ili kujaza nafasi ya madaktari walioingia kwenye mgomo kwa zaidi ya
siku 90 hadi sasa.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
amethibitisha kupokea ombi hilo la Serikali ya Kenya. Hata hivyo,
hakutaka kutoa ufafanuzi zaidi.
“Ndio… lakini tafadhali usiniulize maswali zaidi,” Waziri Ummy anakaririwa na The Citizen.
Hivi
karibuni, Serikali ya Kenya ilitangaza mpango wa kuwaajiri madaktari
kutoka Tanzania, Ethiopia na Cuba kwa lengo la kuziba pengo la madaktari
walioingia katika mgomo nchini humo.
Hata
hivyo, Jumuiya ya Madaktari Tanzania (MAT) kupitia kwa Mwenyekiti wake
mteule, Dkt. Elisha Osati jana kilieleza kuwa hakiungi mkono ombi la
Serikali ya Kenya katika kipindi hiki ambacho madaktari wa nchi hiyo
wako kwenye mgomo.
“MAT
haiungi mkono mpango wa Serikali ya Kenya kuwaajili madaktari wa
Tanzania. Labda kama ombi hili litafanyika baada ya mgomo kuisha,” Dkt. Osati aliandika kupitia mtandao wa Twitter.
Ombi
hilo limekuja ikiwa ni siku chache baada ya MAT kuiomba Serikali
kuwaajiri madaktari kwani kuna zaidi ya madaktari 1500 wapya waliopewa
leseni lakini bado hawajaajiriwa.
Madaktari
wa Kenya wameingia kwenye mgomo wakidai ongezeko la mshahara wa kima
cha chini hadi shilingi milioni 9,700,000 za Tanzania, kiasi ambacho
Serikali ya nchi hiyo imesema haiwezi kumudu.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments