
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na
mazungumzo na Kamishna Jenerali mpya wa Uhamiaji Tanzania Dk. Anna Peter
Makakala,
aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha
rasmi kwa Rais.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alimueleza Kamishna Jenerali Makakala
kuwa Idara ya Uhamiaji Tanzania ni Idara kongwe ambayo imeweza kupata
mafanikio makubwa kutokana na uzoefu mkubwa uliopo kwenye Idara hiyo,
hivyo suala la mafunzo linahitajika ili Idara hiyo iendelee kufanya kazi
kwa wakati uliopo.
Aidha, Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa licha ya mafanikio
yaliopo pia zipo changamoto ambazo kwa mashirikiano ya pamoja zinaweza
kutatuliwa huku akipongeza juhudi za Idara hiyo za kujenga Ofisi mpya za
Makao yake makuu kwa upande wa Zanzibar.
Dk. Shein aliongeza kuwa ipo haja kwa Idara hiyo kuwandaa wafanyakazi
wake kwa kuwapatia mafunzo yanayoendana na kazi zao kwani kazi hiyo
inahitaji mafunzo na utaalamu unaoenda sambamba na kazi hiyo hasa
kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia duniani ambapo Idara hiyo
inapaswa kwenda sambamba na hali hiyo.
Alisisitiza umuhimu wa kuwasikiliza na kuwawezesha wafanyakazi ili
waendelee kuwa na ari ya kufanya kazi zao kwa ustadi na kuweza kupata
mafanikio zaidi ha ikizingatiwa kuwa sayansi na teknolojia imezidi kukua
duniani.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza Mkuu huyo wa Uhamiaji kuwa kuna
umuhimu wa kuendeleza mashirikiano na vikosi vyengine vya ulinzi na
usalama hapa nchini ili Idara hiyo iweze kuendelea kufanya kazi kwa
ufanisi zaidi.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliendelea kutoa pongezi kwa Idara hiyo
kwa kuendelea kufanya kazi vizuri na kwa mashirikiano kati ya
wafanyakazi na viongozi wakuu wa Idara hiyo waliopo Zanzibar na wale
waliopo Tanzania Bara.
Nae Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Tanzania Dk. Anna Peter Makakala
alitoa shukrani kwa Dk. Shein kwa kuendelea kuiunga mkono Idara hiyo na
kumueleza kuwa licha ya kazi zake inazofanya Idara hiyo ya Uhamiaji pia,
ina kazi ya kukusanya mapato.
Kamishna Makakala alieleza kuwa azma ya Idara hiyo ni kuelekea kwenye
teknolojia zaidi na juhudi za makusudi zimekuwa zikiendelea kuchukuliwa
katika kuhakikisha hilo linafanikiwa.
Alieleza kuwa licha ya baadhi ya changamoto zilizopo katika Idara
hiyo ambazo zinaendelea kupatiwa ufumbuzi suala la mafunzo kwa
wafanyakazi wake limepewa kipaumbele kwa kiasi kikubwa.
Aliongeza kuwa Idara ya Uhamiaji ni Idara ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania hivyo itaendelea kufanya kazi zake kwa mashirikiano ya pamoja
katika maeneo yote ya ndani ya Jamhuri hiyo ya Muungano wa Tanzania
yaliopo Tanzania Bara na Zanzibar.
Pia, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji huyo, alimuhakikishia Dk. Shein
kuwa Idara hiyo itaendelea kufanya kazi kwa mashirikiano na vikosi
vyote vya Ulinzi na Usalama nchini Tanzania kwa kutambua umuhimu huo
katika kufikia lengo walilojiwekea katika utendaji wao wa kazi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
chanzo: zanzibar24.
Comments