Daesh latumia gesi ya sumu kujaribu kulizuia jeshi la Iraq kuyakomboa maeneo yaliyosalia Mosul.

Kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) limetumia silaha zenye gesi ya sumu katika kulizuia jeshi la Iraq kusonga mbele katika maeneo yaliyosalia.

Jeshi la Iraq limetangaza kuwa, wanachama wa kundi hilo maarufu kwa kutenda jinai dhidi ya binaadamu limetumia maguruneti yenye gesi ya sumu katika eneo la Badush ambapo jeshi la Iraq kwa kushirikiana na harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'ab lilikuwa linaelekea kwa ajili ya kulikomboa.


Mji wa Badush ambo upo kaskazini magharibi mwa mji wa Mosul, unatajwa kuwa makao makuu ya genge hilo, katikati ya mkoa wa Nainawa (Nineveh.) Jumatano iliyopita harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'ab ilitangaza kuanzisha operesheni kali kuelekea mji wa Badush na kuidhibiti jela ya mji huo. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanachama wa Daesh wametumia makombora yenye gesi ya sumu katika viunga vya mji huo ili kuwazuia askari wa serikali kuudhibiti, njama ambazo hata hivyo hazikufanikiwa.

Katika operesheni kuelekea mji huo, makumi ya magaidi wameangamizwa pia. Wakati huo huo viongozi wa Iraq wametangaza habari ya kutiwa mbaroni makumi ya wanachama wa kundi la Daesh wakiwa baina ya wakimbizi wakati wakijaribu kukimbia kutoka maeneo ya magharibi mwa mji wa Mosul kuelekea meneo ya kusini magharibi ambapo jeshi la Iraq limetia kambi.

Hayo yanajiri katika hali ambayo kiongozi wa kundi hilo la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) Ibrahim al-Samarrai, maarufu kama Abubakr al-Baghdadi, ametoa hotuba ya mwisho akikiri kushindwa kundi hilo nchini Iraq na amewataka wafuasi wake kukimbilia maeneo ya milimani kwa usalama wao au kujiripua

chanzo:parstoday.

Comments