CCM wafikia 300 ubunge Afrika Mashariki.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman KinanaMSIMAMO wa Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kupiga marufuku vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi wowote vimechangia kuibua wagombea lukuki kusaka ubunge katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), baada ya wagombea takriban 300 kujitokeza.

Wagombea wa rika na jinsi mbalimbali waliojitokeza kuchukua na kurudisha fomu, wamepongeza msimamo huo wa Rais Magufuli ambao umewapa fursa maskini na matajiri kuingia katika kinyang’anyiro cha kutafuta tiketi za kuingia EALA.


Msimamo huo wa kuwashughulikia watakaotumia rushwa katika uchaguzi wowote, Dk Magufuli aliutoa kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM uliofanyika mjini hapa, Machi 12, mwaka huu, ambako aliahidi kuwashughulikia wanachama au viongozi watakaotoa au kupokea rushwa kwenye uchaguzi.

Hadi kufikia jana, wagombea zaidi ya 80 walijitokeza kuchukua fomu kupitia CCM kuwa wabunge wa EALA katika kituo cha Dodoma, wengine wengi zaidi ya 200 walichukua Dar es Salaam na wanane wamechukua Zanzibar.

Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni leo saa 10.00 jioni.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti wakati wakirudisha fomu katika chumba cha Katibu Msaidizi Mkuu wa Oganaizesheni Makao Makuu ya chama jana, walisema ukiachia mbali kuwapo kwa fursa hiyo ndani ya chama, suala ya kuzuiwa vitendo vya rushwa kumewapa hamasa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.

Miongoni mwa waliochukua na kurudisha fomu kuchaguliwa kuwa wabunge wa EALA ni vijana wasomi na wenye vigezo wanaofika asilimia 50 na nusu yake ni wasichana.

Uchaguzi huo wa wabunge wa EALA utafanyika Aprili 4, mwaka huu kuchagua wabunge tisa wa kuiwakilisha Tanzania katika bunge hilo lenye makao makuu yake Arusha.

Wagombea wote wanatakiwa kufika ofisi ndogo ya Lumumba, kesho wakiwa na vyeti halisi, baada ya hapo Sekretariati ya Chama Cha Mapinduzi itahakiki vyeti na majina ya watakaopenya yatapelekwa Kamati Kuu (CC) itakayokutana siku chache baadaye.

Wagombea watakaopenya kwenye CC , majina yao yatapelekwa mbele ya wabunge wa CCM na kupigiwa kura watakaoshinda watapelekwa mbele ya Bunge na kuchaguliwa wabunge sita kutoka chama hicho na kuungana na wapinzani watatu na kuwa na wawakilishi wa Tanzania tisa katika EALA.
chanzo;Habarileo.

Comments