Vita ya dawa za kulevya yaingia Zanzibar.

Baada ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuvitupia lawama vyombo vya sheria Zanzibar, wakidai vinachangia kukwamisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Jeshi la Polisi linayo orodha ya watu 42 wanaotuhumiwa kuhusika na uingizaji na uuzaji wa dawa hizo.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Hassan Nassir alisema jana kwamba watuhumiwa hao ambao hakuwataja, wameanza kuhojiwa na wamefanyiwa upekuzi kwenye nyumba zao.



“Tunafahamu kuwa wauza unga ni wajanja kwa kuwa inawezekana wakatupeleka nyumba tofauti na tuzitakazo, lakini tutahakikisha tunafika maeneo yote ambako tunadhani ni vichaka vya biashara hiyo,” alisema.


Alisema polisi haina mpango wa kuwapa taarifa watuhumiwa hao kwa kuwataja majina hadharani na kwamba kazi inayofanyika ni kuwafuata wanakoishi na kuwapa ujumbe wa kuhitajika kwa mkuu wa upelelezi kwa ajili ya mahojiano.



Kamanda Nassir alisema kazi ya kuwahoji watuhumiwa hao ilianza juzi. Kuhusu namna walivyowatambua, kamanda huyo alisema walipata majina yao kutoka kwa watumiaji wa dawa hizo.



“Hii ni kazi ya muda mrefu, tumewatumia watumiaji wa dawa za kulevya katika upelelezi ili kuwapata,” alisema.



Kamanda huyo alikana taarifa kwamba kudorora kukamatwa watuhumiwa kunasababishwa na rushwa ndani ya jeshi hilo kupitia kitengo cha kupambana na dawa za kulevya.



“Pale tunapowakamata watuhumiwa na baada ya kufanya mahojiano tukiwaachia tunaonekana tumechukua rushwa, lakini jamii ielewe kuwa hatuwezi kumtia hatiani mtu hadi ushahidi ukamilike, mkiona hivyo mjue mtu huyo hajaingia moja kwa moja katika hatia,” alisema.



Alisema vituo vya Polisi siyo jela, bali ni sehemu ya kufanya uchunguzi wa awali dhidi ya kesi kwa watuhumiwa, hivyo kuitaka jamii kutofikiria kila mtu anayepelekwa kituoni ni lazima afungwe au ashtakiwe.



Hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed alisema Serikali haitamvumilia mtu yeyote ambaye atabainika kuhusika katika utumiaji, uuzaji, kushirikiana au kuwalinda wahusika wa dawa za kulevya.


Alisema Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesharidhia kuwachukulia hatua za kisheria mara moja wanaobainika kujihusisha na biashara hiyo.



Hatua hiyo ya Polisi Zanzibar, imekuja siku chache baada ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya, Rogers Sianga kueleza mipango na mikakati ya ofisi yake katika kutimiza majukumu yake ambako alisema vita dhidi ya mihadarati siyo ya Dar es Salaam peke yake, bali ya nchi nzima na kwamba itafika hadi Zanzibar kwa sababu ikidhibitiwa Bara na ikaendelea visiwani itakuwa kazi bure.


chanzo:Mwananchi.

Comments