Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye katika maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani
yaliyofanyika mwanzoni mwa wiki katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya habari nchini.
Alisema kuwa wakati umefika kwa wadau wa sekta ya habari kufikiri kwa
kina namna ya kuhabarisha umma kwa kuangalia namna ya uwasilishaji
ambapo kwa sasa changamoto kubwa ni kasi ya ukuaji wa teknolojia ya
habari na namna ambapo redio zinaweza kushindana na vyombo vingine.
Alisema kwa wanahabari wanapaswa kuwa makini na taarifa wazitoazo kwa
jamii kwani kumekuwa na mazoea ya baadhi yao kuripoti habari bila
kufanya uchuinguzi wa kina huku wakitumia chanzo kimoja cha habari
badala ya kujiuliza maswali mengi ili kupata taarifa sahihi.
Akizungumzia urasimu wa upatikanaiji wa habari mikoani, wilayani na
wizarani alisema kuwa Sheria ya Habari imempa nguvu Mkurugenzi wa Habari
Maelezo amabaye ndiye msemaji mkuu wa serikali awajibike kutoa habari
za serikali.
Alisema kuwa kwa kipindi cha nyuma maofisa habari walikuwa
hawahudhurii kwenye vikao muhimu vya maamuzi, hivyo kutokuwa na taarifa
sahihi. Alisema kuwa kama waziri mwenye dhamana na wizara hiyo lengo la
serikali ni kuhakikisha kunakuwa na mazingira wezeshi kwa ukuaji wa
tasnia ya habari hata kama ni kwa kubadilisha sheria inayobana uhuru wa
habari.
Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii
Tanzania-COMNETA, Prosper Kwizige alisema kuwa ipo changamoto kwa baadhi
ya maafisa habari mikoani na wilayani kuleta urasimu mkubwa katika
utoaji wa taarifa zinazohitajika kwa waandishi wa habari hivyo
kukwamisha upatikanaji wa habri kwa umma.
Kwa upande wake, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk
Edefonce Nfuka alisema kuwa maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa muafaka kwa
wadau wa sekta hiyo kutoa mrejesho wa wahitimu kutoka kwenye vyuo hapa
nchini na hivyo kusaidia katika uboreshaji wa mitaala ili kuwa na
wahitimu mahiri kwenye sekta hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk Ayubu
Rioba alisema kuwa kwa siku za nyuma redio ilikuwa ni chombo cha
kuaminika katika utoaji wa habari hivyo kujijengea umaarufu na kuaminika
zaidi tofauti na ilivyo sasa ambapo kuna upotoshaji mkubwa.
chanzo:Habarileo.
Comments