Akizungumza na HabariLeo siku moja baada ya kumalizika kwa kongamano
hilo, Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi, alisema ameshapokea maombi
kutoka mikoa kadhaa ambayo inahitaji pia kupata jukwaa kama
lililofanyika Simiyu Februari 13 mwaka huu.
“Kuna watu wanashangaa kwamba kampuni ya magazeti imefanikiwa vipi
kuandaa kitu kama hiki,
lakini sisi tumedhamiria kuandaa mambo mengi
zaidi ya haya,” alitamba Dk Yonazi akiwa mwenye furaha baada ya jukwaa
hilo la kwanza na la aina yake kufanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Dk Yonazi alidokeza, hata hivyo, kwamba mikoa itakayofuata baada ya Simiyu ni pamoja na Dodoma, Arusha, Dar es Salaam na Mwanza.
Kadhalika alidokeza kwamba wadau wengine zaidi wameonesha kutaka
kushiriki katika majukwaa yatakayoandaliwa na TSN siku za usoni.
Mhariri huyo Mtendaji alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony
Mtaka kwa kuwa mwepesi kukubali kufanyika kwa jukwaa hilo la kwanza
mkoani kwake, na kushiriki kikamilifu katika kulifanikisha.
Mapema, Mtaka alielezea kufurahishwa na ujio wa jukwaa hilo mkoani
kwake akisema: “Hili ni jukwaa muhimu sana kwetu, jukwaa linalokutanisha
taasisi za fedha, Mamlaka ya Mapato, Baraza la Uwekezaji la Taifa na
wadau kutoka makundi mbalimbali.Kwa mkoa wa Simiyu ambao tunajenga
mabadiliko makubwa ya kiuchumi, hili jukwaa kwetu lina afya sana."
Wadau wengine waliosaidia kufanikisha jukwaa hilo lililoandaliwa na
TSN, wachapishaji wa magazeti ya serikali ya HabariLeo, SpotiLeo na
Daily News na kutoa mada mbalimbali ni pamoja na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Benki ya NMB, Benki za TIB Development na TIB Corporate
na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).
Kufuatia uwepo wa taasisi hizo muhimu kwa maendeleo, washiriki
waliibua hoja lukuki baada ya mada mbalimbali kuwasilishwa ambazo
zilisaidia kupata ufahamu katika masuala mbalimbali ya biashara, ulipaji
wa kodi na fedha, hususani namna ya kupata mikopo.
Katika jukwaa hilo ambalo ‘mtoto alikuwa hawezi kutumwa dukani’
kutokana na mada motomoto zilizowasilishwa, washiriki walikaa kuanzia
saa tatu asubuhi hadi saa mbili usiku bila kuonekana kuchoka.
Mikoa mingi yataka kushirikiana na TSN Mtaka asifiwa kwa kuona mbali TIB: Ibueni fursa mpate mikopo Karibuni kuwekeza Simiyu.
chanzo:Habarileo.
Comments