Alitoa mwito huo wakati akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho
pamoja na wananchi wanaoishi maeneo ya jirani katika kijiji cha Matufa,
wilayani Babati akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Manyara.
“Mkurugenzi wenu amesema hapa kuwa ni vigumu kwa wakulima kupata
mikopo na pia mikopo ya benki ina riba kubwa. Napenda niwasisitize kuwa
msiogope kukopa kwa sababu hakuna tajiri duniani aliyeendelea bila
kukopa,” alisema.
Aliwaeleza kuwa zipo benki ambazo zinatoa mikopo kwa wakulima ambazo
ni Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), NMB, CRDB, Benki ya Kilimo (TADB)
na Benki ya Rasilimali (TIB). “Benki ya Kilimo TADB inatoa mikopo kwa
wakulima na pia kuna TIB Corporate na TIB Development,” alifafanua.
Aliwataka wakurugenzi wa kiwanda hicho waharakishe uagizwaji wa
mitambo mipya ili kiwanda hicho kiweze kuongeza uzalishaji wake. Alisema
takwimu za mahitaji ya sukari hapa nchini zinapaswa kupitiwa kwa sababu
hazitoi picha halisi.
“Tanzania ina watu milioni 50 lakini mahitaji ya sukari tunaambiwa ni
tani 420,000 kwa mwaka. Wenzetu wa Kenya wako milioni 45 lakini
mahitaji yao ni tani 800,000 kwa mwaka. Tulishawaambia wapitie upya hizi
takwimu zao.”
Mapema, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Ofisa Uhusiano wa
kiwanda hicho, Dipak Odedra alisema kiwanda hicho kilianzishwa mwaka
2006 kikiwa na uwezo mdogo wa kusaga tani 50 za miwa kwa siku lakini
sasa kina uwezo wa kusaga tani 500 kwa siku.
“Kuongezeka kwa uzalishaji na kukua kwa kiwanda kumechangiwa na
mikataba ya kuwashirikisha wakulima wadogo kuwakopesha mitaji tangu
kutaarisha mashamba, kupanda mbegu, usafiri na utaalamu lengo likiwa
kununua miwa yao inapokuwa tayari kuvunwa,” alisema.
Alisema mpango huo shirikishi wa kupanda miwa unahusisha vijiji zaidi
ya 10 ambapo jumla ya ekari 1,150 zinalimwa na wakulima wadogo
waliohamasika na kuona faida za kilimo hicho. Alisema mwaka jana kiwanda
hicho kilisaga tani 64,584 za miwa na kuweza kuzalisha tani 4,251 za
sukari.
“Kwa msimu ujao baada ya kufunga mitambo ya kisasa, tumepanga
kuongeza uzalishaji ili tuweze kusaga tani za miwa 650 kwa siku kutoka
tani 500 za sasa. Na mwaka kesho tunataraji kufikisha tani 750 za miwa
kwa siku,” aliongeza.
chanzo:Habarileo.
Comments