Madiwani hao walitoka nje ya ukumbi wa mkutano, baada ya Meya Mwanyemba kukataa kumpisha katibu wa madiwani aongoze kikao.
Madiwani hao wanamtuhumu Mwanyemba kwa ubadhirifu wa Sh milioni 30 za mradi wa maji wa Zuzu.
Akizungumza na kwa niaba ya madiwani 47 wa chama, Naibu Meya wa
Manispaa hiyo, Jumanne Ngede alisema mradi huo wa maji ulilenga
kuuwanufaisha wakazi wa kata ya Zuzu, lakini utekelezaji wake umekuwa
ukisuasua kutokana na kugubikwa na ubadhirifu wa fedha za mradi huo.
Ngede ambaye ni diwani wa Chamwino alisema kutokana na tuhuma hizo
kumkabili Meya Mwanyemba, madiwani 43 kati ya 47 wa chama, walisaini
karatasi ya kutokuwa na imani naye na kuwasilisha pamoja na barua kwa
Mkurugenzi ya Manispaa wakilalamikia mstahiki meya huyo.
Kwa upande wake, Diwani wa Ipagala, Gambo Dotto ambaye alisaini barua
kwa niaba ya madiwani wenzake wa chama ya kumtaka meya asiwe mwenyekiti
wa kikao chao, alitaja tuhuma nyingine kuwa ni pamoja na kutumia
madaraka vibaya, kushiriki katika vitendo vya rushwa, kushindwa
kutekeleza majukumu yake vizuri na kuwadanganya madiwani kwa makusudi na
kupandikiza chuki za uongo miongoni mwao.
“Tunachotaka sisi madiwani si kumvua umeya, bali tunataka asiwe
mwenyekiti wa vikao vya madiwani wa chama katika kipindi hiki ambacho
uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo ukiendelea,” alisema Dotto.
Dotto alimtaka meya kwa heshima na busara asiongoze vikao, hivyo
kwani akiwa mwenyekiti wa kikao, wajumbe wanaweza kupandwa na jazba
dhidi yake, hawatakuwa na uhuru kujadili hoja zilizopo mbele yake na
yeye mwenyewe anaweza kutumia vibaya nafasi ya uenyekiti na kuamua mambo
vibaya.
Dotto alisema, madiwani hao walimtaka meya asiongoze vikao vyao
kutokana na kutajwa na mkandarasi wa mradi huo, Kampuni ya Kalago
Investment Limited mara baada ya kufikishwa polisi kutokana na kushindwa
kutekeleza mradi huo, ambao ulikuwa ukisuasua, ndipo akamtaja meya
kwamba wanashirikiana naye katika ubadhilifu wa fedha hizo.
Dotto alisema mradi huo umegubikwa na utata mwingi ukiwamo ya
kutofuata taratibu kanuni za zabuni tangu kutangaza, kufungua na,
kusaini mikataba na hadi kampuni kupewa tuzo ya zabuni hiyo, kitendo
ambacho kilifanyika kwa siku moja na siku iliyofuatwa fedha zilichotwa
hata kabla Kamati ya fedha haijafanyia kazi mkataba huo.
Dotto alisema madiwani wanashangaa meya huyo kwa kitendo cha kuamua
kurudisha Sh milioni 30 kwa kupitia kampuni yake ya Mdegela
International Co Limited na kudai risiti ya fedha hizo, wakati yeye
hakuwa mkandarasi wa mradi na ametajwa tu kwamba anahusika na
haijathibitika kwamba amezitumia.
Alipoulizwa na madiwani kwamba kwanini anarudisha fedha wakati
anatuhumiwa kuhusika tu, Mwanyemba alidai kwamba anataka kujenga sifa
nzuri ya manispaa hiyo, hivyo anaona bora arudishe fedha hizo kwa lengo
la kuendeleza uelewano uliokuwa wa madiwani ndani ya manispaa hiyo.
Mkurugenzi wa Manispaa, Godwin Kunambi alikiri kupokea barua
waliyoandika madiwani wa CCM na kusainiwa nao 43 na ameifanyia kazi kwa
kumwandikia Meya ajibu tuhuma hizo dhidi yake ndani ya siku 5 tangu jana
Februari 20, mwaka huu.
“Nilimwandikia Mstahiki Meya barua yenye kumbukumbu no HMD/CC
20/2/vol 111/77 ya Februari 20, mwaka huu, nikimtaka ajibu kwa maandishi
kuhusu tuhuma hizo dhidi yake katika muda wa siku tano tangu jana,”
alisema Kunambi.
Kunambi alisema anasubiri majibu ya tuhuma hizo kutoka kwa Meya na
akiyapata, yatapalekwa kwa Mkuu wa Mkoa, Jordan Rugimbana kwa hatua
zaidi.
Mwanyemba alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo dhidi yake, alidai
kwamba yeye hawezi kuzungumza lolote kutokana na kwamba yupo ndani ya
kikao pamoja viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri
Mkuu, anayeshughulikia Ajira, Kazi na Vijana, Antony Mavunde.
Kutokana na mradi huo kugubikwa na utata tangu mwanzo, Injinia wa
Maji wa Manispaa, Sasala amesimamishwa kutokana na kusaini mkataba wa
mradi huo, wakati kisheria mkataba huo unasainiwa na mwanasheria wa
serikali ni injinia wa maji.
chanzo:Habarileo.
Comments