Karibuni kuwekeza Simiyu-RC.

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, amesema mwekezaji yoyote mwenye mradi unaoleta tija kwa jamii, anakaribishwa mkoani kwake na kwamba atapewa ardhi bure.

Mtaka alikuwa anazungumza na gazeti hili, siku moja baada ya kufanyika kwa Jukwaa la Uchumi mkoani kwake lililoandaliwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kwa kushirikiana na ofisi yake na pia kuwashirikisha wadau kadhaa wa maendeleo.


Alisema anajua kuna maeneo Dar es Salaam si rahisi kupata ardhi bure, lakini Simiyu huu ndio muda wa watu kuchangamkia ardhi kwa ajili ya uwekezaji na kwamba kinachotakiwa ni uwekezaji huo uwe na faida kwa jamii, hususani kutoa ajira kwa vijana.

Alisema wamedhamiria kuhakikisha Simiyu inakuwa miongoni mwa mikoa mitano nchini inayoongoza kwa viwanda.

“Tunachoamini ni kwamba haiwezekani kujenga uchumi wa viwanda Tanzania kama tutaendelea kubaki na Dar es Salaam ileile, Mwanza ileile, Arusha ileile, Mbeya na Morogoro ileile... Lazima tuongeze mikoa mingine ya kufanana na hiyo mikoa mikubwa, ili tafsiri ya mwananchi kuhusu uchumi wa kati ianze kuonekana,” alisema mkuu huyo wa mkoa kijana.

Wadau wengine waliosaidia kufanikisha jukwaa hilo lililoandaliwa na TSN, wachapishaji wa magazeti ya serikali ya HabariLeo, SpotiLeo na Daily News ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki ya NMB, Benki za TIB Development na TIB Corporate, na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

chanzo:Habarileo.

Comments