MKUU wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Ali Hapi amepiga
marufuku viongozi wa mitaa kuhamishia nyaraka za serikali katika nyumba
zao binafsi kwa kuwa ni kinyume cha sheria na watakaokaidi watachukuliwa
hatua za kisheria.
Agizo hilo la mkuu wa wilaya kwa wenyeviti na watendaji wa mitaa na
kata ya wilaya hiyo limekuja baada ya kupata taarifa ya kuwepo kwa
mgogoro kuwa katika Mtaa wa Malindi, Kata ya Mbweni uliosababisha kuwepo
kwa ofisi mbili moja, ikiwa ni ya serikali na nyingine ikiwa nyumbani
kwa Mwenyekiti wa Mtaa huo, Bariki Elibariki.
Hapi alimtaka mwenyekiti huyo na Mtendaji wa Mtaa huo, Abdallah
Mkeyenge kukaa chini na kumaliza tofauti zao ambazo kwa sasa zimefikia
katika hatua mbaya ya kutoleana lugha za vitisho na kudhalilishana
hadharani.
“Hili suala la ofisi ya serikali kuwa nyumbani kwa mtu binafsi
haikubaliki hata kidogo na kuna waraka ulitolewa na mkurugenzi kupiga
marufuku suala hilo. Nyaraka za serikali haziwezi kukaa kwa mtu binafsi
labda kama hiyo ni ofisi yako na mkeo, hilo halituhusu,” alisema Hapi.
Alisema uhusiano mbaya wa viongozi wa mtaa huo yamekuwa
yakiwadhalilisha viongozi hao jambo ambalo linawachafulia sifa zao,
hivyo waone umuhimu wa kumaliza migogoro yao binafsi.
Amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda
kufuatilia suala hilo kwa ajili ya kubaini ukweli ili hatua za kisheria
zichukuliwe.
“Watendaji ni waajiriwa wa serikali, mwenye mamlaka nao ni
Mkurugenzi, Mwenyekiti huna mamlaka ya kumkataa au kumhamisha kwa sababu
humtaki, unatoa taarifa kwa mwajiri wake na mkurugenzi ndio anachukua
hatua juu yake,” alisema mkuu wa wilaya.
Aliongeza kuwa ana taarifa maeneo mengi ya wazi yameuzwa na watu
mbalimbali akiwemo kiongozi mstaafu ambaye hakumtaja, jambo ambalo ni
kinyume cha sheria huku akitaka jamii kulinda maeneo hayo.
Awali, akitoa taarifa ya kata, Mtendaji wa Kata ya Mbweni, Kuluthum
Msimike alisema kata hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
uhaba wa watendaji wa mitaa ambapo alisema kuna mitaa mitano, lakini
watendaji ni wawili.
Msimike alisema katika Mtaa wa Malindi Estate kuna ofisi mbili ambapo
moja ni ya serikali na nyingine iko nyumbani kwa mwenyekiti wa mtaa
huo, jambo ambalo limekuwa likichangia kudidimia maendeleo ya mtaa huo.
Katika ziara hiyo, Hapi alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo
ikiwemo Shule ya Msingi Kiumbageni, ambako alitoa siku saba kwa ofisi ya
Ofisa Elimu wa Manispaa hiyo kuhakikisha anaongeza idadi ya walimu
katika shule hiyo na hasa walimu wa awali.
Alisema wilaya hiyo ina ziada ya walimu hivyo ni jambo la ajabu kuona
baadhi ya shule zina upungufu wa walimu huku akitaka mwakilishi wa
Ofisa Elimu, Fatma Mwiru kuhakikisha anafanya utaratibu wa kuongeza
walimu katika shule hiyo.
chanzo:Habarileo.
Comments