
Hivyo Dk. Shein aliwataka wananchi na wanaCCM kuepuka kauli za upotoshwaji zinazosambazwa mitandaoni.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa CCM, Mkoa wa Mjini iliopo Amani mara baada ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa vijana kwa ajili ya maandalizi ya Ligi ya Mpira wa Miguu kwa Timu 18 za Unguja.
Katika maelezo hayo Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar anayoiongoza yeye itaendelea kuwa madarakani na kueleza kuwa mazungtumzo aliyoyafanya leo kati yake na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni mazungumzo ya kawaida baada ya kumwita kwa lengo la kubadilishana mawazo na kueleza changamoto zilizopo katika Majimbo yao.
Dk. Shein alisema kuwa yeye akiwa ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi pia, ni sehemu ya Baraza hilo na kwenda kuzungumza na Wajumbe wa Baraza hilo sio jambo jipya kwani ameshawahi kufanya hivyo kutokana na taratibu na kanuni zilizopo.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwasisitiza wanaCCM na wananchi kuwa hakuna Baraza linalovunjwa asubuhi hivyo kauli hizo zinazozungumzwa na zinazosambaa ni za upotoshaji na zisizo na ukweli.
Aidha, Dk. Shein aliwaeleza wanaCCM wakiwemo vijana waliohudhuria katika hafla hiyo kuwa Mihimili mitatu iliyopo ikiwemo Mahakama, Serikali na Baraza la Wawakilishi hakuna muhimili hata mmoja unaomshurutisha mwenziwe bali hufanya kazi kwa mashirikiano ya pamoja ili kufikia malengo yaliokusudiwa katika nchi.
Nae Balozi Seif Ali Idd alieleza kuwa uzushi unaosambazwa katika mitandao hauna maana na kueleza kuwa amepokea simu nyingi kutoka kwa wananchi kutokana na kauli hizo za mitandaoni ambazo si za msingi kuwa Dk. Shein leo anakabidhi nchi kwani maneno hayo hayakuanza leo bali ni kawaida kwa wapinzani.
Hivyo aliwataka wanaCCM na wananchi kupuuza kauli hizo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
chanzo:zanzibar24.
Comments