Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar,
wakati alipofanya mazungumzo na Mabalozi Wateule wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania,
waliofika Ikulu kumuaga Rais pamoja na kufanya nae
mazungumzo ambapo alisisitiza kuwa sekta ya viwanda imepewa kipaumbele
na kutiliwa mkazo mkubwa na Serikali zote mbili.
Miongoni mwa Mabalozi hao ni Balozi Emmanuel John Nchimbi ambaye
anakwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Brazil, Balozi Mbelwa Brighton
Kairuki anaekwenda nchini China, Balozi Geogre Kahema Madafa anaekwenda
Italy, Balozi Profesa Elizabeth Kiondo anakwenda nchini Turkey.
Wengine ni Balozi Dk. James Alex Msekela UN nchini Geneva, Balozi
Samwel William Shelukindo anaekwenda Paris, France na Balozi mteule Lt.
Jeneral (Mstaafu) Paul Ignance Mella anaekwenda D.R. Congo.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa shabaha kuu ya Serikali
zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar ni kuimarisha sekta ya viwanda vikiwemo viwanda vikubwa,
vidogo na vya kati hivyo ni vyema wakatumua fursa hiyo kuwakaribisha
wawekezaji wa nchi hizo wanazokwenda kufanyia kazi.
Akizungumzia kwa upande wa Zanzibar, Dk. Shein alisema kuwa licha ya
Zanzibar kuwa ni visiwa ambavyo vimezungukwa na bahari sambamba na
kuwepo ukanda wa bahari kutoka Tanga hadi Mtwara lakini maeneo hayo
hakuna viwanda vya samaki ambayo ni bidhaa inayotokana na bahari.
Alieleza kuwa eneo la bahari la Zanzibar ni maarufu sana kwa samaki
aina ya jodari ambaye ni samaki anaependwa duniani lakini wamekuwa
hawavuliwi ipasavyo na badala yake hutokea meli kubwa za kigeni za uvuvi
ambazo huja kuwavua kwa njia za wizi.
Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa
kuimarisha sekta ya ajira na kupunguza changamoto iliyopo katika sekta
hiyo hapa nchini hasa kwa vijana.
Aidha, Dk. Shein alieleza haja ya Mabalozi hao kuitangaza Zanzibar na
Tanzania nzima kiutalii ambapo kwa upande wa Zanzibar sekta hiyo
imekuwa ni muhimu kutokana na kuchangia asilimia 80 ya pato la Taifa.
Dk. Shein alieleza kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
ifikapo mwaka 2020 ni kupokea watalii zaidi ya laki tano kutokana na
mikakati iliyopo hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar inavivutio vingi vya
kitalii.
Pia, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuvitangaza vivutio vya kitalii
vilivyopo nchini vikiwemo Mbuga za wanyama, sehemu za kihistoria, fukwe
na vyenginevyo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwatakia heri na fanaka Mabalozi hao
katika utendaji wao wa kazi kwenye Balozi hizo na kueleza kuwa kwa vile
anatambua utendaji wao wa kazi ana matumaini makubwa kuwa watatekeleza
vyema dhamana zao hizo.
Nao Mabalozi hao walimthibitishia Dk. Shein kuwa wamepokea maelekezo
yote aliyowapa na kuahidi kuyafanyia kazi hasa kwa maeneo maaluma ya
Zanzibar na Tanzania Bara.
Akitoa maelezo kwa niaba ya Mabalozi wenziwe, Balozi wa Tanzania
nchini Brazil Balozi Emmanuel John Nchimbi, alimuhakikishia Dk. Shein
kuwa watafanya kazi kwa juhudi kubwa na maarifa kwa maslahi ya nchi yao
na wananchi wake.
Balozi Nchimbi kwa niaba ya wenziwe walitoa pongezi na shukurani kwa
kwa Rais Dk. Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
John Pombe Magufuli kwa kuteuliwa kwenda kuiwakilisha Tanzania katika
nchi hizo.
Mabalozi hao walimuhakikishia Dk. Shein kuwa katika wadhifa wao huo
juhudi za makusudi watazichukua kwa mashirikiano ya pamoja katika
kuhakikisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo na Tanzania
unaimarishwa zaidi sambamba na kuimarisha maslahi kwa pande zote mbili
za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
chanzo:zanzibar24.
Comments