Alitoa kauli hiyo juzi wakati akizumgumza na mamia ya wakazi wa mji
wa Orkesumet, wilayani Simanjiro akiwa katika siku ya pili ya ziara yake
mkoani Manyara.
Alisema serikali imepanga kuiombea fedha za kazi ya ujenzi wa
barabara hiyo yenye urefu wa km 430 kwenye mkutano ujao wa bajeti na
kwamba imepanga kutafuta wakandarasi wengi na kuwagawa kwa vipande ili
barabara hiyo ijengwe kwa kipindi kifupi.
“Barabara yenu nimeiona. Imo kwenye Ilani ya CCM. Ujenzi wake
utaanzia Arusha –Mbauda – Simanjiro – Kiteto hadi Kongwa. Rais John
Magufuli ameahidi kuwa Serikali hii haitawaangusha na itawahudumia
wananchi wote bila kujali itikadi za kisiasa,” alisema.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa maji kwenye mji wa Orkesumet ambao
ni Makao Makuu ya wilaya ya Simanjiro, Waziri Mkuu alisema serikali
inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji kutoka Ruvu
hadi kwenye mji huo.
Kuhusu upatikanaji wa umeme, Waziri Mkuu aliwahakikishia wakazi hao
nia ya Serikali ya kufikisha umeme katika vijiji vya wilaya hiyo.
“Serikali imeamua kupeleka umeme kwenye vijiji 8,000 na kati ya
hivyo, vijiji vya Simanjiro vimo… serikali imepanga kufikisha umeme
kupitia miradi ya REA.
Wakandarasi wameshapewa kazi, na sasa wameenda kutafuta vifaa.
Tumeamua hivi sasa kama kuna vijiji vya mbali na line ya umeme, au ni
gharama sana kuwapelekea umeme kwa sababu ya umbali, hao ni lazima
wapatiwe umeme wa sola na tutaweka sola katika kila nyumba,” alisema.
Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo Mei 30, mwaka huu kazi hiyo iwe imekamilika katika wilaya ya Simanjiro.
Akizungumzia kuhusu migogoro ya ardhi ambayo iliandikwa kwenye
mabango, Waziri Mkuu alimtaka Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhandisi Zephania
Chaula afuatane na Ofisa Ardhi wa Wilaya na waende kwenye vijiji husika
kusikiliza malalamiko ya wananchi hao.
Akifafanua kuhusu baadhi wa watu kujimilikisha maeneo makubwa ya
ardhi, Waziri Mkuu alisema Sheria ya Ardhi namba 5 inaainisha kuhusu
umiliki wa ardhi na kwa Serikali ya Kijiji hairuhusiwi kutoa ardhi zaidi
ya ekari 50.
chanzo:Habarileo.
Comments