Shule zenye maabara kupewa vifaa vyote.

SHULE za sekondari 1,629 ambazo maabara zake zimekamilika kujengwa nchini, zitapatiwa vifaa vyote vya maabara vilivyonunuliwa na serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 16 ifikapo mwisho wa mwezi huu.
Aidha, katika kuhakikisha uboreshaji wa elimu unazidi kuimarika nchini halmashauri zimetakiwa kurekebisha ikama ya walimu kwa kuwa imekuwa changamoto kubwa kutokana na kukosekana kwa uwiano wa walimu katika shule zilizopo kwenye halmashauri moja.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amesema hayo jana wakati wa hafla ya kuzipongeza halmashauri 10 zilizofanya vizuri katika utekelezaji wa Mpango wa Lipa kulingana na Matokeo.
Profesa Ndalichako amesema, katika juhudi za serikali kuboresha sayansi ya teknolojia nchini wameweza kukabiliana na ukosefu wa maabara kwa serikali kuagiza vifaa hivyo vya shule 1,629 ambavyo vimeagizwa nje ya nchi na vitapokewa nchini mwisho wa mwezi huu.
Amesema, katika kuhakikisha hilo, pia vifaa kwa ajili ya elimu maalumu vyenye thamani ya Sh bilioni 3.6 vimeshaingia nchini na wanamalizia taratibu za kutoa bandarini.
Alisema vifaa hivyo ni kwa ajili ya wasioona, wenye matatizo ya usikivu, vifaa kwa ajili ya wenye ualbino pamoja na vifaa vya kupima viwango vya uhitaji maalumu kwa lengo la kuwapima watoto mapema na kuchukua hatua.
Akizungumza katika hafla hiyo ambayo Halmashauri ya Kaliua mkoani Tabora imeongoza kupata Sh bilioni 704.4 baada ya kushika nafasi ya kwanza, Profesa Ndalichako aliagiza fedha walizopewa zinazotoka kwa wadau wa maendeleo zitumike kwa urekebishaji wa Ikama ya walimu katika halmashauri, ujenzi wa madarasa na vyoo pamoja na ukamilishaji wa maabara.
Halmashauri zilizofuata ni Muleba Sh milioni 681.2, Geita Sh milioni 657.9, Bunda Sh milioni 538.1, Rorya Sh milioni 419.3, Nzega Sh milioni 415.2, Ngara Sh milioni 384.7, Itilima Sh milioni 364.3, Kongwa Sh milioni 363 na Chato Sh milioni 336.2 ambayo pekee ilikuwepo katika halmashauri zilizofanya vizuri mwaka jana katika programu hiyo ambayo huzipatia fedha halmashauri zote, lakini kwa kukidhi vigezi na halmashauri iliyopata fedha ndogo imepewa Sh milioni 74.
“Nasisitiza halmashauri kutumia fedha hizo kulingana na vipaumbele vilivyobainishwa kwa kuzingatia taratibu za matumizi ya fedha za serikali na kuhusisha jamii katika miradi iliyotajwa kwani fedha hizo zinafanyiwa ukaguzi kwani mwaka jana halmashauri chache hazikufuata utaratibu,” alisema na kuwataka kutumia vyanzo vyao vya fedha kurejesha fedha za programu hiyo huku wakisitishiwa kupewa fedha za mwaka huu mpaka watakapomaliza kuweka sawa ukaguzi huo.
Waziri huyo alisema programu hiyo ilizinduliwa Septemba, 2014 chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) inayotekelezwa kwa miaka minne hadi Septemba, 2018 na inatekelezwa kwa Sh bilioni 550 ambazo tofauti na programu nyingine serikali inapata fedha kutoka kwa wafadhili baada ya kutekeleza vipaumbele vilivyokubaliwa.
Alibainisha kuwa lengo ni kuinua ubora wa elimu msingi hivyo fedha hizo hutolewa kwa kukidhi vigezo katika maeneo sita ambayo ni upatikanaji wa fedha, uimarishaji wa mfumo wa menejimenti ya Habari za Elimu, usawazishaji na upangaji Ikama ya walimu katika halmashauri, utekelezaji mikakati ya kipaumbele, utoaji wa takwimu na matokeo ya elimu.
chanzo;habarileo.

Comments