Serikali kushirikiana na vyombo vya habari.

SERIKALI imeahidi kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari nchini katika kutoa habari kwa ajili ya kuhabarisha umma kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo serikali katika kutekeleza majukumu yake.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametoa ahahi hiyo jana alipotembelea na kujionea utendaji kazi wa Kampuni ya IPP Media kwenye vituo vya Televisheni vya ITV, EATV na Capital Tv.
Waziri Nape pia ametembelea kampuni ya Sahara Media inayomiliki kituo cha Star TV na Redio Free Africa tawi la Dar es Salaam.
Ameahidi kuendeleza ushirikiano baina ya serikali na vyombo vya habari katika utoaji wa habari ambazo ni muhimu kwa wananchi kujua, zikiwemo hatua ambalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kutekeleza majukumu yake katika kuwaletea wananchi maendeleo.
“Niseme kwa kipindi cha nyuma kumekuwa na urasimu wa utoaji wa taarifa muhimu kutoka kwetu kuja kwenu vyombo vya habari, lakini niwahakikishe kuwa sasa serikali imefungua milango kwenu na tuendelee kushirikiana katika kuhabarisha umma wa Watanzania,” amesisita Nape.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas amevihakikishia vyombo vya habari nchini ushirikiano mzuri katika kupata habari za serikali kutoka katika vitengo vyote vya mawasiliano serikalini.
Dk Abbas amesema, kwa sasa wako katika mpango wa kuboresha vitengo vya mawasiliano serikali ili kuboresha upatikanaji wa habari zinazohusu serikali.
“Niwahakikishieni ndugu zangu wanahabari kuwa suala la upatikanaji wa habari kutoka serikali litakuwa si la kusumbuana tena na tunatengeneza mfumo katika vitengo vyote vya mawasilaino serikalini ili iwe rahisi kupata taarifa kutoka kwetu,” amesitiza Dk Abass.
Mkurugenzi Mtendaji wa ITV/Radio One, Joyce Mhavile ameishukuru serikali kwa kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari vya binafsi nchini katika kutoa taarifa kwa umma ambazo zimesaidia kuelimisha, kuburudisha na kutengeneza mazingira ya watu kuamini yale yanayotolewa na vyombo vyao.
Mkuu wa Sahara Media kwa upande wa Dar es Salaam, Cyprian Musiba ameipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa vyombo vya habari nchini na kuahidi kuongeza ushirikiano baina yao na serikali katika upashanaji habari.
Nape yupo katika ziara ya siku sita, kutembelea vituo vya televisheni kujionea utendaji kazi wa vituo hivyo ikiwa pamoja na changamoto zilizopo ili kupata namna bora ya kuiendeleza sekta ya habari kwa manufaa ya taifa.
chanzo;habarileo.

Comments