Dk. Shein aliyasema hayo kwa nyakati tofauti alipokutana na uongozi
wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa (KOICA) ukiongozwa na Makamu wa
Rais wa KOICA pamoja na kufanya mazungumzo na uongozi wa Seoul
Broadcasting System (SBS TV), Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar inathamini juhudi hizo za Mashirika hayo ya Korea katika
kuunga mkono harakati za maendeleo hapa Zanzibar na kueleza kuwa mradi
wa skuli ya Kwarara ni wa mwazo katika miradi ya elimu ambayo haijawahi
kutokea.
Dk. Shein alisema kuwa Tanzania na Jamhuri ya Korea zilianza
mahusiano ya Kidiplomasia mnamo mwaka 1999 ambapo nchi hiyo imeweza
kuisaidia Tanzania ikiwemo Zanzibar mambo mbali mbali ikiwemo sekta ya
elimu, kuimarisha kilimo cha mpunga, kilimo cha umwagiliaji maji na hivi
karibuni mradi wa kufuga samaki nao unatarajiwa kuanza.
Katika mradi huo mpya wa kufuga samaki Dk. Sgein alisema kuwa umradi
huo utazalisha vifaranga vya samaki na majongoo ya bahari huko
Beit-el-Rais mradi ambao utagharamiwa na KOICA.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Korea kupitia
mashirika yake hayo kwa ujenzi wa skuli mpya ya kisasa na ya aina yake
huko Kwarara inayotarajiwa kufunguliwa kesho (11.1.2016) ambapo alisema
hiyo ni ishara ya urafiki kati ya nchin hiyo na Zanzibar.
Nao uongozi wa KOICA umetoa pongezi kwa Dk. Shein kwa mafanikio
makubwa yaliofikiwa hapa Zanzibar na kuahidi kuendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu.
Shirika la SBS lilieleza kuwa mikakati yao ni kujenga skuli mia moja
katika bara la Afrika na skuli hiyo ya Kwarara ni ya Miamoja kati ya 99
ambazo wamejenga katika nchi nyengine ila kwa upande wa skuli hiyo ni ya
kipekee kutokana na kuwa na studio na mambo mengine ya habari, mradi
ambao KOICA nao wamesaidia kwa asilimia 50.
Sambamba na hayo, Shirika la KOICA linatarajia kutoa msaada wa dola
za Kimarekani milioni 10 ambazo zitapitia kwa Shirika lisilo la
Kiserikali la Korea kwa ajili ya kuimarisha elimu ya Sekondari kwa
wanafunzi wa kike.
Aidha, Shirika la Good Neighbors Tanzania wamekubali kujenga skuli ya
msingi huko Kwarara itakayokuwa na madarasa 24 ambapo tayari eneo la
skuli hiyo limeshapatikana.
Pamoja na hayo, KOICA imeahidi kuunga mkono katika miradi mengine
mipya itakayoianzisha hapa Zanzibar huku wakitumia fursa hiyo kutoa
shukurani kwa mashirikiano mazuri waliyayapata kutoka kwa Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Amali.
Shirika la SBS TV limeadihi kuitangaza Zanzibar nchini mwao sambamba
na kuutangaza utamaduni wa Zanzibar kutokana na vipindi maalum vya
Televisheni watakavyovitengeneza ambapo pia uongozi huo ulimpongeza Dk.
Shein kwa juhudi zake za kuchapa kazi .
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk.
chanzo; zanzibar24.
Comments