Aidha, gazeti hili limetakiwa kuzibeba ajenda za serikali na
kuziwasilisha kwa wananchi, ili wapate taarifa kamili kuhusu utekelezaji
wa ajenda hizo, ambazo ni pamoja na viwanda, hali ya utamaduni wa nchi,
urithi na sanaa.
Gazeti hili linatolewa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN)
inayochapisha Daily News na Spotileo, ambalo jana liliadhimisha miaka 10
tangu kuanzishwa kwake Desemba 21, 2006.
Akizungumza wakati wa sherehe hizo, Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alisema alipozungumza na Dk Magufuli
asubuhi ya jana kwa njia ya simu kuhusu maadhimisho hayo, Rais
alibainisha wazi kuwa anajivunia gazeti hilo kwa kazi nzuri linayofanya.
“Nikiwa njiani wakati nakuja kuhudhuria maadhimisho haya,
nilizungumza na mwenye gazeti hili, Rais wetu Dk John Pombe Joseph
Magufuli na kumwelezea bayana kuhusu maadhimisho haya.
Amenipa salamu
zake na ameniambia niwaambie kuwa anajivunia sana kazi nzuri inayofanywa
na gazeti hili,” Nape alimkariri Rais Magufuli. Alisema Rais
ameipongeza timu nzima ya Kampuni ya TSN kwa kumsaidia kuwafanya
Watanzania waendelee kuwa na amani.
“Pia amenituma niwaambie kuwa
amepanga kufanya ziara kwenye kampuni yenu, lakini kwa kushtukiza,
hakuniambia siku wala saa, jiandaeni,” aliongeza Nape.
Akizungumzia gazeti hili, Nape alisema HabariLeo ni gazeti pekee la
Kiswahili la serikali, lililopewa dhamana na jukumu la kuihabarisha
jamii kwa kutumia lugha fasaha ya Kiswahili, lakini pia kuwa kiunganishi
baina ya serikali na wananchi wake.
“Ujio wa HabariLeo umekuwa na mchango mkubwa sana katika juhudi za
kuepuka migawanyiko ya kisiasa nchini, na kuimarisha juhudi za
kuendeleza umoja wa kitaifa.
Hili likiwa ni mojawapo ya malengo ya
msingi na kusudio la kuanzishwa kwa gazeti hili na kwa kweli niwapongeze
kwa namna mlivyolifanya kwa kiwango cha juu kabisa,” alisisitiza.
Alisema gazeti hilo linaendelea kutoa habari kwa ukweli na uhakika
bila kupendelea upande wowote, linaimarisha misingi ya umoja na
mshikamano wa Watanzania bila kujali tofauti zao za kiitikadi, kidini,
rangi wala kabila.
Nape alibainisha kuwa jambo kubwa na ambalo linaweza lisipatikane
katika magazeti mengine ni mtawanyiko wa habari kutoka sehemu mbalimbali
za nchi.
“Nikisoma HabariLeo naweza nikapata hata habari za kijijini kwetu,
nikapata habari za mbali kabisa tofauti na vyombo vingi ambavyo wakati
mwingine unapata habari za mijini peke yake,” alibainisha waziro.
Alilitaka gazeti hili kuhakikisha linabeba ajenda za serikali kama
vile suala la kuijenga Tanzania ya viwanda ili wananchi waelewe vyema
ajenda hizo na kushiriki katika kuzitekeleza.
“Kwa mfano ajenda ya viwanda, takribani asilimia 80 ya wananchi
wanategemea kilimo, katika ajenda hii wanatakiwa kuhabarishwa na
kuelimishwa ili washiriki vyema na kunufaika,” alisisitiza, na kuongeza
kuwa gazeti hili pia linaweza kuibeba ajenda ya hali ya utamaduni wa
Tanzania, urithi na sanaa ili Watanzania waelewe vyema ajenda hizo na
kusaidia nchi hiyo isipoteze utamaduni wake.
Alisema anatamani kuiona HabariLeo ya miaka 10 ijayo, inaweza kufika
katika maeneo yote nchini na kuangalia namna ya kupenya kwenye taasisi
mbalimbali na inamudu ushindani wa soko la kwenye mitandao.
“Mimi kama mteja nisilazimike kubeba nakala halisi ya gazeti lenyewe
na hili pengine si mimi tu ninayependa; bali wapo watu wengine wengi
wanatamani kusoma HabariLeo kupitia mitandao ya kijamii.
Najua mmeanza
vizuri lakini kuna umuhimu wa kuangalia namna ya kuingiza mitandao mingi
zaidi ya kijamii kwa lengo la kuruhusu kufika kwa wateja wenu wengi kwa
kuzingatia ukuaji wa teknolijia ya habari na mawasiliano,” alifafanua.
Aidha, Nape aliwataka wafanyakazi wa HabariLeo na TSN kwa ujumla,
kuhakikisha wanachapisha habari zenye mwelekeo wa kuona nchi inaendelea
kuwa ya amani na utulivu na pia inaendelea kuwa na umoja na mshikamano.
Kwa upande wake, Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi alisema
anashukuru kuwa mmoja wa viongozi wa kampuni ya TSN, anayeshuhudia
kutimiza miaka 10 kwa moja ya magazeti ya kampuni hiyo, la HabariLeo,
ambalo kwa sasa linatekeleza wajibu wake kama ilivyo lengo la kuanzishwa
kwake.
Alisema gazeti hili limejizatiti katika kuwahabarisha wananchi, hasa katika yale wanayoyaelewa na si yale yanayosemwa.
Alisisitiza kuwa kwa sasa gazeti hilo, limeingia katika mkakati wa
kuandika habari za kiuchunguzi ili kuisaidia serikali, itambue mambo
yanayoendelea, ikiwemo kushiriki katika utungwaji wa sera za serikali.
“Ndio maana msimamo wa HabariLeo umezingatia sana katika kuhimiza
maendeleo na kuleta matumaini, limekuwa ni gazeti la kijamii,
likijitofautisha na mengine kila inapowezekana,” alisisitiza.
Dk Yonazi alisema gazeti hili, limeongeza wigo wa serikali wa
kuwasiliana na watu wake na linatumika kama daraja kati yake na
wananchi, kwa kupewa dhamana ya kuhabarisha, kuelimisha, kuburudisha na
pia kuhoji mambo mbalimbali ya serikali, katika chama tawala cha CCM na
wananchi.
Alitaja kazi za gazeti hili kuwa ni kuanika na kudodosa mambo,
yanayofanywa na mamlaka kuelekea uchumi wa kati na kuwasilisha maoni ya
wananchi kuhusu mikakati hiyo, hasa Dira ya mwaka 2025 inayoweka wazi
vipaumbele vya serikali.
Alisema pamoja na kwamba gazeti hili linakabiliwa na changamoto
nyingi, ikiwemo ushindani mkubwa katika soko, mabadiliko ya teknolojia
na mabadiliko katika lugha ya Kiswahili, bado linatumia fursa hizo
kujipambanua na kuendelea kuhabarisha wananchi.
Alitaja mipango ya kampuni ya TSN katika kujiimarisha zaidi kuwa ni
pamoja na kuanzisha huduma ya ushauri huku ikiendelea na huduma yake ya
sasa, kuchapisha magazeti ya serikali ya Daily News, Sunday News,
HabariLeo, Habari- Leo Jumapili na Spotileo.
Katika maadhimisho hayo, TSN pia ilisaini mkataba na Baraza la
Kiswahili Tanzania (BAKITA) wa kushirikiana katika kukuza Kiswahili
kupitia HabariLeo.
Mkataba huo ulisainiwa na Dk Jim Yonazi na Katibu Mtendaji wa Bakita,
Dk Seleman Sewangi. Akizungumzia mkataba huo, Dk Yonazi alibainisha
kuwa TSN imejipanga kupaisha Kiswahili kwa kuhakikisha watanzania
wanapata taarifa zilizoandikwa kwa lugha fasaha, lakini pia kuelimishwa
juu ya matumizi ya lugha hiyo na baraza hilo.
“Si ajabu kupitia gazeti hili kuchapishwa majarida na vitabu
vinvyotumia lugha fasaha ya Kiswahili. Kupitia mkataba huu Bakita
watatusahihisha, watatukosoa,” alisema.
Dk Sewangi alisema kupitia mkataba huo, baraza hilo litakuwa linatoa
maneno ambayo hutumiwa kwa ufasaha ili kuwajengea uelewa zaidi wananchi
kuhusu lugha ya Kiswahili.
Mhariri Mtendaji wa zamani wa TSN, Isaac Mruma alilipongeza gazeti
hili kwa kuwa gazeti la kwanza nchini linaloandika kwa kutumia lugha ya
Kiswahili na si kutumia lugha ya Kiswahili kuandika.
chanzo;habarileo.
Comments