Posho hizo ni za posho za mazingira magumu, kujenga uwezo na
vitafunwa katika halmashauri za wilaya na manispaa zote nchini. Badala
yake, ametaka posho hizo zitumike kwenye miradi ya maendeleo.
Kutokana na agizo hilo, kwa jiji la Dar es Salaam pekee zaidi ya Sh
bilioni 130 zilizokuwa zikilipwa kwa halmashauri na manispaa za jiji
hilo kwa posho mbalimbali, zitaokolewa na kuingizwa kwenye miradi na
shughuli za maendeleo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu huyo ametoa siku tatu kwa
watumishi wa umma 10, wanaotakiwa kuripoti katika halmashauri na
manispaa mpya ya Kinondoni, kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi.
Vinginevyo, watakuwa wamejifukuzisha kwenye utumishi wa umma.
Alisema hayo alipozungumza na watumishi wa Halmashauri na Manispaa ya
Kigamboni jijini Dar es Salaam jana katika ziara yake ya siku moja ya
kujitambulisha na kukumbushana kuhusu uwajibikaji. Majaliwa aliitaka
kila halmashauri hiyo, ifanye tathmini ya mahitaji ya kila kata na
kusimamia maendeleo.
Alisema katika halmashauri kumekuwa na matumizi ya fedha nyingi
kinyume na taratibu na kanuni. Matumizi hayo huwanufaisha wachache, huku
wengine ambao nao waliwajibika wakinyimwa fursa ya kunufaika na wao.
“Utakuta hadi mlinzi anahangaika katika suala zima la ukusanyaji wa
mapato ya halmashauri, lakini mwisho wa siku vitafunwa huliwa na
wachache wanaojiita wakubwa huku wengine wakisikilizia kwa nje,”
alisema.
Alitolea mfano manispaa za Ilala, Temeke na Ubungo kuwa kiasi cha
fedha za posho kinacholipwa kwa ajili ya vitafunwa kwa mwaka ni Sh
milioni 600, pamoja na posho za mazingira magumu jumla ni Sh milioni 960
kwa kila manispaa.
Kwa upande wa Kinondoni, alisema manispaa hiyo pamoja na vitafunwa
ambavyo ni zaidi ya Sh bilioni moja kwa mwaka, pia hulipa posho ya nyuma
kwa wakuu wa vitengo kwa mwaka ambayo ni Sh bilioni 2.8.
“Nafuta hizi posho zote ambazo hazitambuliki kisheria, naagiza
kuanzia leo malipo haya yapelekwe kwenye shughuli za maendeleo. Naonya
Mkurugenzi yeyote nitakayebaini amelipa watu wake posho hizi,
amejifukuzisha kazi mwenyewe,” alisisitiza.
Aidha, aliagiza kuwa kiasi cha Sh 800,000 kinachotolewa kwa kila
diwani kwa ajili ya kufanya uhamasishaji wa maendeleo kwenye kata yake,
kuanzia sasa kisitolewe moja kwa moja kwa diwani, bali kipelekwe kwenye
kata na kufuatiliwa namna kinavyotumika.
Pamoja na hayo, Waziri Majaliwa alionya halmashauri zote kuhakikisha
kuwa kila fedha inayopelekwa kwenye halmashauri hizo, inatumika kama
ilivyokusudiwa. Endapo itabainika kutumika kwa shughuli nyingine,
wahusika watachukuliwa hatua.
“Narudia nataka hili lieleweke,kila fedha itakayopelekwa kwa
halmashauri itumike kwa lengo lililokusudiwa. Kama ni fedha ya ujenzi wa
madarasa iende kwenye ujenzi wa darasa na uendane na thamani ya fedha
yenyewe na si vinginevyo,” alisema.
Pamoja na hayo, Kiongozi huyo pia alibainisha kuwa serikali ya awamu
ya tano, haitambeba tena mtumishi wa umma yeyote, anayevunja maadili ya
utumishi wa umma au anayekosa nidhamu kwa kumhamisha kituo, bali kuanzia
sasa mtumishi huyo atafukuzwa kazi.
Aliwataka watumishi wote wa umma nchini, kuwajibika ipasavyo kwa
kuhakikisha wanamtumikia vyema mwananchi, ikiwa ni pamoja na kuepuka
vishawishi na kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa.
“Juzi nilipokuwa Longido, nilikuta mtumishi mmoja amesababisha hasara
ya takribani Shilingi bilioni 1.2. Baada ya kujua ameharibu, akaomba
uhamisho wa kwenda Bahi, tukamzuia, sasa hili ni fundisho, serikali
haimbebi tena mtu anayeharibu kazi yake. Hapohapo ulipoharibu ndio
tunapomalizana,” alifafanua.
Kuhusu maslahi ya watumishi wa umma, Waziri Majaliwa alisema serikali
imejipanga kuboresha maslahi ya watumishi wote wa umma na ndio maana
imeunda timu maalum, kwa ajili ya kuhakiki viwango vya mishahara
vinavyotolewa ili kujua kama vinaendana na hali ya maisha.
Aidha, alisema serikali hiyo pia inataka kuondokana na tatizo la
malimbikizo ya fedha za watumishi wake, kwa kulipa malimbikizo yote
yanayodaiwa na watumishi.
Akizungumzia suala la kupokelewa na mabango ya wananchi kila
anapokwenda, Majaliwa alisema kuanzia sasa popote atakapoenda, akikutana
na mabango, kiongozi yanayomhusu ajiandae kumpatia majibu, kwa kuwa
hiyo ni alama ya kutowajibika kwake.
“Ukiona nimepokewa na mabango wewe kama ni kiongozi yasome mapema
ujipange kunipa majibu, maana hii ni indication kuwa watu hawathamaniwi
mpaka wamsubiri waziri Mkuu ndipo wasikilizwe. Tatueni kero za wananchi
wenu kabla hawajanifikia,” alionya.
Akizungumzia watumishi 10 walioshindwa kuripoti katika vituo vyao vya
kazi katika halmashauri na manispaa ya Kigamboni, Majaliwa alisema
kitendo cha watumishi hao, kushindwa kuripoti bila kutoa taarifa ni
dalili kuwa hawataki tena kuwa watumishi wa umma.
“Nawapa siku tatu waripoti wenyewe kabla hawajiachisha kazi, na kama kuna mtu anawazuia awaachie mara moja,” alisema Majaliwa.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa wakati
akiwasilisha taarifa ya wilaya hiyo, alibainisha kuwa mpaka sasa
takribani asilimia 98 ya watumishi wa umma waliotakiwa kuhamia kwenye
halmashauri hiyo wameripoti kazini isipokuwa watumishi hao 10 ambao
hakuna taarifa zozote juu yao.
chanzo;habarileo.
Comments