Aidha, amesema ajali zilizotokana na matumizi mabaya ya taa za magari zimeongezeka kutoka 104 mwaka 2015 hadi 123 mwaka jana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu matumizi ya taa za gari, Kamanda Mpinga alisema matumizi kusudiwa ya taa kadiri ya mfumo wake yanahusiana na usalama barabarani na ndiyo maana Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 iliyofanyiwa Marekebisho 2002 kwa kutambua umuhimu wake katika kifungu cha 39(1) na 39 C inatoa ufafanuzi wa kisheria juu ya matumizi sahihi ya gari barabarani.
Kamanda Mpinga alisema yapo magari hususan magari makubwa ya mizigo na hata ya abiria ambayo yamefanyiwa marekebisho kwa kuongeza taa ambazo hazikuwekwa na mtengenezaji na huzitumia taa hizo kuhatarisha usalama barabarani.
“Taa hizi hutumika vibaya hasa nyakati za usiku na kuwa chanzo cha ajali kwa kuwa zinapotumika hupoteza uwezo wa mtumiaji mwingine wa barabara kuona mbele. Taa hizi hazina uwezo wa kuzitawala kwa maana ya kubadilisha uwakaji wake kutoka beam light na kuwa full,” alieleza.
Alisema taa hizo zikiwashwa huwaka moja kwa moja hivyo ni kinyume cha sheria kufunga taa hizo katika gari na ni hatari zaidi hasa zinapotumika bila kujali watumiaji wengine wa barabara.
Alisema ni marufuku gari kufungwa taa za aina yoyote zenye mwanga mkali pamoja na ‘sports light’ kwani taa hizo zimekuwa hatari kwa watumiaji wa barabara kwa kuwa hupoteza uwezo wa dereva mwingine kuona mbele.
“Nasisitiza taa hizo ziwe za kiwandani au za kuongeza ziondolewe katika magari yote yaliyofungwa taa hizo na kwa watakaokaidi hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa na kuziondoa mara moja…nawashukuru watumiaji wa barabara ambao wameunga mkono usimamizi wa sheria kwa kuziondoa taa hizo,” alisema.
chanzo;habarileo.
Comments