Aidha chama hicho kimemuomba Rais John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), Ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na
vyombo vingine vinavyohusika, kuchukua hatua za dharura za kuokoa fedha
hizo.
Hata hivyo, Sakaya ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF upande wa Bara,
alisema fedha hizo hazijaibiwa kama ambavyo inadaiwa, isipokuwa kwa
nafasi aliyonayo ndani ya chama alimuandikia Msajili kuomba fedha hizo
kwa ajili ya chama kuingia katika uchaguzi, ndipo zikaingizwa katika
akaunti hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam jana,
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, Julius Mtatiro alisema CUF imeibiwa Sh
369,378,502.64 za ruzuku.
“Fedha hizo zilitoroshwa kutoka Hazina ya Serikali Januari 5 mwaka
huu na kuingizwa kwenye Akaunti ya NMB tawi la Temeke yenye jina la The
Civic United Front ikiwa na akaunti namba 2072300456,” alisema Mtatiro.
Alisema katika tukio hilo la wizi, Hazina imetorosha ruzuku hiyo kwa
kumuamini Lipumba, Sakaya, aliyekuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la
CUF, Thomas Malima na genge lao ambao walishavuliwa uongozi na pia
uanachama.
Hata hivyo, Mtatiro alisema kuwa baada ya kugundua utoroshwaji huo,
CUF imejiridhisha kuwa akaunti ambayo Hazina wameshiriki kuitumia
kutorosha fedha za umma na mali ya CUF ni akaunti ya CUF, ambayo
hutumiwa na Wilaya ya Temeke kwa ajili ya kupokea mgawo wa ruzuku kutoka
kwa Chama Taifa.
Aidha, Mtatiro alisema vikao vya kitaifa vya CUF, yaani Kamati ya
Utendaji ya Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, havikuwahi
kupitisha maamuzi yoyote kwamba fedha za CUF ziwekwe katika akaunti hiyo
ya wilaya iliyoko NMB Temeke.
Mtatiro alisema siku mbili kabla ya utoroshaji wa fedha hizo,
ulisukwa mpango wa kuwaondoa baadhi ya viongozi wa CUF wa Wilaya ya
Temeke kwenye utiaji saini unaoihusu akaunti tajwa; na kuwafanya watu wa
Profesa Lipumba kuwa watia saini, ambao ni Sakaya na Malima.
Alisema watia saini hao wapya, waliulizia kiasi cha fedha kilichomo
kwenye akaunti hiyo na walifanya hivyo katika tawi la NMB Mandela Road.
Alisema kesho yake, wakiongozwa na Malima walikwenda katika Benki ya
NMB tawi la Temeke na wakatoa Sh milioni 69 na kuhamisha Sh milioni 300
kwenda kwenye akaunti ya mtu binafsi kwenye akaunti ya NMB 41401600207
ikimilikiwa na Diwani wa CUF wa Handeni mkoani Tanga.
“Mtu huyu ni wa karibu na Lipumba na ni mmoja kati ya wanachama
wanane waliosimamishwa uanachama na Baraza Kuu, jana (juzi) akaunti hii
ilikuwa kwenye mchakato wa kuondoa fedha hizo kutoka kwenye akaunti
hiyo, na kubaki na Sh 207,907 tu,” alisema Mtatiro.
Alisema mtu huyo alitoa Sh milioni 100 kutokea Benki ya NMB tawi la
Magomeni, kisha akiwa hapo Magomeni akatoa Sh milioni 50, tawi la
Kariakoo alitoa Sh milioni 100 na mwisho akatoa tena Sh milioni 49.5
huku wakiwa na ulinzi wa polisi na gari ya chama hicho akiwa na Sakaya
na wengine.
“Hadi tuongeavyo sasa miezi mitano CUF inadai ruzuku ya Shilingi
milioni 635 na kwa kuwa fedha zilizotoroshwa Hazina zimepelekwa kwenye
akaunti isiyotambuliwa Bodi ya Wadhamini ya chama inatamka kuwa hadi
sasa ruzuku yake ni Shilingi 635,000,000,” alisema Mtatiro.
Ntatiro alisema Bodi ya Wadhamini ya CUF inakutana na pia Kamati ya
Utendaji ya Taifa ya CUF pia kwa ajili ya kutafakari tukio hilo kubwa la
chama na kuelekeza hatua za kiutawala na kisheria za kuchukua haraka.
Akizungumza na gazeti hili jana, Sakaya alisema chama kimepata nafasi
ya kushiriki uchaguzi mdogo katika kata 14 kati ya 20 za Tanzania Bara,
hivyo fedha zinahitajika kwaajili ya maandalizi hayo hivyo aliamua
kumuandikia Msajili kuomba fedha.
“Hizo fedha hazijaibwa wala nini, hao wanaoongea hawajui wanaongea
nini, mimi niliandika barua kwa nafasi yangu kulingana na uchaguzi
tulionao mbele yetu nikaomba hizo fedha na zimetolewa kwaajili ya
kusambazwa zinakohitajika,” alisema Sakaya ambaye alisema yuko jimboni
kwake.
Sakaya alisema taarifa zilizotolewa na Mtatiro, hazina ukweli na
kwamba Mtatiro hana nafasi yoyote ndani ya chama. Alisema ukweli ni
kwamba Msajili kuweka fedha kwenye akaunti hiyo ya tawi la Temeke ni
sahihi, kwani ana maamuzi ya kuweka popote ili mradi zinaingia katika
akaunti zinazomilikiwa na chama.
Aidha alisema pia kuwa ni kweli fedha hizo zimetolewa na ni kwa ajili
ya kusambazwa katika halmashauri ambazo zinahitajika kuendelea na
kampeni za uchaguzi. Uchaguzi huo mdogo wa viti vya udiwani utafanyika
Januari 22 mwaka huu.
Lipumba pamoja na viongozi na wanachama wengine 10 Agosti mwaka jana
walisimamishwa uanachama na Baraza kuu la Uongozi la Taifa lililokutana
katika kikao cha dharura huko visiwani Zanzibar hata hivyo maamuzi hayo
yalitenguliwa na Msajili wa vyama vya Siasa.
Kikao hicho pia kilimteua Mtatiro kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Uongozi itakayokuwa na wajumbe wawili ambao ni Katani Ahmed Katani na
Severina Mwijage, ambayo itafanya kazi za Mwenyekiti na Makamu
Mwenyekiti hadi hapo utakapoitishwa Uchaguzi mwingine wa kujaza nafasi
hizo.
chanzo;habarileo.
Comments