Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Balozi Seif Ali Iddi, wakati akizungumza na viongozi wa chama hicho katika Kata ya Mtoni kwenye Jimbo la Temeke,Unguja.
Balozi Seif alisema huu ni wakati muafaka kwa viongozi kusimamia na kutekeleza Ilani ya CCM ambayo ni mkataba kati ya chama na wananchi katika kuleta maendeleo.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya watendaji wameyapa kisogo malengo hayo na sasa wapo katika mchakato wa kupanga safu na kutafuta wagombea wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Alisema CCM inafahamu mpango huo na kuwajua viongozi wa aina hiyo. Kimesema dawa yao ipo jikoni inachemka.
“CCM haifurahishwi na baadhi ya viongozi ambao kazi yao kubwa ni kujenga makundi kwa ajili ya urais wa mwaka 2020. Chama kina kazi ya kutekeleza na kusimamia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015- 2020 ya kuleta maendeleo kwa wananchi na si kupanga safu ya wagombea urais,” alieleza Mjumbe huyo wa Kamati Kuu.
Alisema viongozi watakaobainika kufanya matukio ambayo ni kinyume na mikakati na malengo ya chama watachukuliwa hatua.
“Wembe uliotumika mwaka 2015 kwa ajili ya kupata safu ya wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tutautumia kwa upande wa Zanzibar kupata mgombea wa urais mwaka 2020,” alisema.
Balozi Seif alisema wapo baadhi ya viongozi wasaliti ambao walithubutu kununua kadi kwa kuwashirikisha wapinzani ili wapate nafasi za uongozi.
Aliwataka viongozi wa chama wa nyadhifa mbalimbali ikiwemo Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kusimamia majukumu yao vizuri, ikiwemo kutekeleza Ilani ya Uchaguzi na ahadi zao kwa wapiga kura ili kukiweka chama katika nafasi nzuri ya kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.
chanzo;habarileo.
Comments