Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inakemea vikali
vitendo vya ukeketaji vinavyotaarifiwa kufanyika katika Kata ya Kivule,
Manispaa ya Ilala jijini Dar es salaam, na mikoa mengine ambayo
imekaririwa na vyombo vya habari.
Wizara
inaagiza wazazi na walezi kuacha mara moja vitendo vya ukeketaji kwani
ni ukatili, husababisha madhara kwa watoto wa kike na wasichana ni kosa
la jinai.
Athari
za ukeketaji kwa wahanga ni pamoja na kusababisha majeraha kwa watoto,
vifo, vilema, maradhi kama fistula na mengineyo. Watoto wa kike na
wanawake wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa vitendo vya ukeketaji bila
ridhaa yao na wakati mwingine ridhaa hiyo huwa imepatikana kwa hila,
jambo ambalo ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Wizara
inatoa rai kwa vyombo vya dola kuwakamata wazazi, walezi, mangariba, na
wote wanaoendeleza vitendo vya ukeketaji dhidi ya watoto wa kike na
wasichana katika kata ya Kivule na maeneo mengine nchini, na kuwafikisha
mahakamani ili sheria iwezekuchukua mkondo wake.
Wizara
itaendelea kupambana na vitendo vya ukeketaji vinavyotaarifiwa katika
jamii zetu, na itaongeza juhudi ya utoaji elimu kwa jamii sambamba na
kuwachukulia hatua wote wanaojihusisha na mila potofu ya ukeketaji.
Wito
unatolewa kwa kila mwananchi kushiriki katika kuzuia vitendo vya
ukeketaji na hasa kufichua matukio ya ukeketaji, na kutoa ushahidi
mahakamani ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki.
Wizara
inatoa rai kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii
katika Mikoa, Halmashauri na Kata katika maeneo ambako kunaarifiwa
kuwepo vitendo vya ukeketaji kuhakikisha kuwa wanashirikiana na mamlaka
husika kuzuia ukatili huo katika nchi yetu.
Erasto T. Ching’oro
Msemaji wa Wizara-Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto
21/12/2016
chanzo;mpekuziblog.
Comments