Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine
Mahiga (Mb) anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa
Mawaziri wa Afrika na Korea unaotarajiwa kufanyika nchini Ethiopia
tarehe 06 na 07 Desemba, 2016 mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Mkutano
huu ambao umeandaliwa na Serikali ya Korea kwa kushirikiana na Umoja wa
Afrika una lenga kukuza ushirikiano pamoja na kuandaa maeneo mapya ya
ushirikiano baina ya Korea na mataifa ya Afrika katika miaka mitatu
ijayo.
Tanzania
ni moja ya nchi nne (4) za Afrika ambazo Korea imezichagua kuanzisha
mahusiano ya kimkakati “strategic partnership” yatakayozifanya nchi hizo
kupewa kipaumbele katika kupokea misaada na mikopo nafuu kutoka Korea
katika kipindi cha miaka mitano ijayo kati ya 2016 hadi 2020.
Katika
kipindi hicho Tanzania itapokea kiasi cha dola za Kimarekani milioni
300 ikiwa ni asilimia 17.1 ya msaada utakaotolewa Barani Afrika, hivyo
kuifanya Tanzania kuwa nchi inayoongoza Barani humo kupata msaada wa
Jamhuri ya Korea.
Pamoja
na ushiriki kwenye Mkutano huo, imependekezwa ufanyike mkutano baina ya
Tanzania na Serikali ya Korea kuzungumzia masuala ya ushirikiano baina
ya nchi zetu mbili.
Aidha,
ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano wa Afrika na Korea ni fursa muhimu
ya kukuza mahusiano baina ya nchi zetu mbili hususan katika Nyanja ya
uchumi. Serikali ya Korea ilitoa ahadi ya kuongeza uwekezaji Barani
Afrika hususan katikasekta za nishati, miundombinu na viwanda.
Itakumbukwa
kuwa, tayari Jamhuri ya Korea inashirikiana na Tanzania katika miradi
mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Mradi wa kuendeleza kilimo cha Mwani
Zanzibar wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 3.6 na Awamu ya
Pili ya Mradi wa kuboresha Uchunguzi wa Afya ya Uzazi Jijini Dar es
Salaam wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni nne (4).
Miradi
mingine ambayo Jamhuri ya Korea inashirikiana na Tanzania ni ujenzi wa
Daraja la Selander Jijini Dar es Salaam, Mradi wa Daraja la Kikwete
kwenye Mto Malagarasi Mkoani Kigoma na Ujenzi wa Hospitali ya Kimataifa
iliyopo eneo la Mloganzila Jijini Dar es Salaam.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 01Desemba, 2016.
chanzo;mpekuziblog.
Comments