Sungura Amtikisa Mbatia .....Amtaka Ajiuzulu Nafasi ya Mwenyekiti NCCR-Mageuzi ili Kukinusuru Chama.
Aliyekuwa
Mkuu wa Idara ya Kampeni ya Chama cha NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura,
amenzisha fukuto kwa kumtaka Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia
kujiuzulu nafasi yake kwa madai kuwa ameshindwa kukiongoza chama hicho
tangu alipoingia madarakani.
Sungura
anasema bila kufanya hivyo, atashirikiana na wanachama wengine
kumwondoa, kwa sababu amekisahau chama na kujikita katika shughuli
nyingine zisizo na tija, jambo ambalo limechangia chama hicho kupata
mbunge mmoja kwenye uchaguzi uliofanyika Oktoba, mwaka jana.
Anasema
hali ilipofikia hivi sasa, chama hicho kinaweza kufa na kubaki historia
ambayo haiwezi kuwasaidia wanachama wengine wanaopigania uhuru na
demokrasia ndani ya nchi yao.
“Hatumwondoi
Mbatia kwa sababu tunamchukia, bali tunamwondoa kwa kushindwa kuangalia
masilahi ya chama na kujikita kwenye shughuli zisizo na tija, jambo
ambalo limechangia kupoteza wabunge na kubaki na mbunge mmoja ambaye
ndiye yeye katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana.
“Kwa
sababu nafasi ya uenyekiti si ubatizo na wala si kiungo cha mwili wake,
hata tuseme tutamuumiza, hivyo basi tunaamini vijana wenye mapenzi mema
na chama wataungana na mimi kuhakikisha kuwa mwenyekiti anatoka
madarakani ili tuweze kukiendesha chama,”- Sungura.
Anadai
kuwa lengo lao ni kufanya siasa zenye tija, zikiwamo za kuzunguka
mikoani kutafuta wanachama wapya na kuandaa viongozi ambao wataweza
kukisimamia chama hadi uchaguzi ujao wa mwaka 2020.
Anasema
kutokana na hali hiyo, nafasi yake itakabidhiwa kwa mwanachama mwingine
kama alivyonyang’anywa mwenzake na kijiti kukabidhiwa yeye ili aweze
kukiongoza chama.
Sungura alijunga na chama hicho tangu mwaka 1992, akiwa mwanachama mwenye kadi N0. 00011763.
Ofisa
Utawala wa chama hicho, Frolian Mbeo, alipoulizwa kuhusu kauli ya
Sungura, alisema hadi jana mchana hakuwa na taarifa yoyote ya kuwapo
malalamiko ya mwanachama huyo.
Alisema
uamuzi wa Sungura, umekuja baada ya kutolewa kwenye nafasi ya
ukurugenzi wa kampeni, jambo ambalo limemfanya kuzunguka mikoani na
kuanza kukisema vibaya chama.
chanzo;mpekuziblog.
Comments