Sakata la kuvuja mitihani Chuo cha fedha Chwaka: wanafunzi wataka kujua hatma yao.

Baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika chuo cha uongozi wa fedha Chwaka wameulalamikia uongozi wa chuo hicho kwa kuwasimamisha na kuwazuia kufanya mitihani kwa madai ya kufanya udanganyifu.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi katika viunga vya chuo hicho kilichopo chwaka wilaya ya kati Unguja, wanafunzi hao wamesema kuwa kitendo cha kuwasimamisha kufanya mitihani kwa madai ya kuvuja bila ya kuwa na ushahidi si cha kiungwana na kinawanyima fursa za kuonyesha uwezo wao bila ya kujua hatma yao ya masomo katika siku za baadae.

Aidha wanafunzi hao wamesema kuwa licha ya kuwepo hatua za kudhibiti mitihani katika Taasisi mbalimbali za Elimu, hatua zinazochukuliwa zinawagusa wanafunzi kwa kiasi kikubwa huku uongozi na walimu ambao wana dhamana kubwa ya udhibiti wa mitihani kutochukuliwa hatua yoyote.

Hata hivyo wanafunzi hao wameiomba serikali pamoja na jamiii kuingilia kati suala hilo ili wapate nafasi ya kuendelea tena na masomo iwapo wataonekana hawana hatia.

Uongozi wa chuo hicho haukua tayari kuzungumza chochote kuhusu tukio la kuzuiwa masomo wanafunzi hao na Afisa mmoja wa chuo hicho amedai kuwa taarifa zinapatikana Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Tunguu.

chanzo; zanzibar24.

Comments