Rais Magufuli na mkewe Mama Janet wakabidhi msaada wa Sh mil 5 ya matibabu ya Mtoto anayeotwa na nyama kichwani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli jana
tarehe 5 Desemba, 2016 wamekabidhi msaada wa Shilingi Milioni 5 kwa
ajili ya kusaidia matibabu ya mtoto Haidari Bonge mwenye umri wa miaka 9
anayesumbuliwa na tatizo la kuota nyama kichwani, kinywani na machoni.
Fedha
hizo zimekabidhiwa kwa Mama wa mtoto huyo Sauda Kassim na Kaimu
Mnikulu Ndugu Ngusa Samike kwa niaba ya Rais Dokta Magufuli katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo mtoto huyo anapatiwa matibabu.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi fedha hizo, Kaimu Mnikulu Ndugu Ngusa Samike alisema
Rais Dkt. Magufuli ameguswa baada ya kutazama kipengele cha Hadubini
“Habari kwa Kina” kilichorushwa hewani katika taarifa ya habari saa 2
usiku na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) tarehe 03 Desemba, 2016.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya ngozi Dkt. Andrew Foi alisema
mtoto Haidari anayeishi Mbagala Kuu Jijini Dar es Salaam alianza kuota
nyama miezi mitatu baada ya kuzaliwa na amekuwa akifanyiwa upasuaji wa
kuondoa nyama hizo mara kwa mara.
Dkt. Foi alisema
Hospitali ya Taifa Muhimbili inatoa matibabu ya mtoto huyo bure tangu
awasili hospitalini hapo isipokuwa kwa matibabu ambayo hayapatikani
hospitalini hapo ndio analazimika kuyalipia katika sehemu husika.
Alisema
mtoto Haidari anahitaji eneo maalum la kuishi muda wote ambalo lina
giza na kuvaa nguo nyeusi zinazomfunika mwili wote ili kujikinga na
miale ya jua ambayo imekuwa ikimuathiri kwa kiasi kikubwa.
Mama wa mtoto Haidari, Ndugu Sauda Kassim alimshukuru
Rais Dkt. Magufuli na mke wake Mama Janeth Magufuli kwa moyo wa upendo
waliouonesha baada ya kuguswa na shida zinazomkabili mtoto wake na kutoa
msaada huo na hivyo kuomba wananchi wengine waige mfano wa Rais na
Mkewe katika kumsaidia mwanawe.
Tayari
mtoto Haidari Bonge, ameshafunguliwa akaunti katika Benki ya CRDB tawi
la Azikiwe yenye namba 0152236450100, ambapo benki hiyo kupitia kwa
meneja Uhusiano wake Godwin Semunyu amekabidhi shilingi laki Tano ikiwa
ni msaada kutoka Benki hiyo.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam.
chanzo;mpekuziblog.
Comments