Mkuu
wa Wilaya ya Mvomero, Mohamed Utali ametoa agizo kwa Mkurugenzi
Mtendaji wa halmashauri hiyo, Florent Kyombo kutomhamisha mwalimu yeyote
kwa kigezo cha cheti cha ndoa.
Alisema
baadhi wanaghushi vyeti hivyo na vya maradhi ili wapate nafasi ya
kufundisha kwenye shule zilizopo kando mwa barabara kuu na mijini hivyo
kusababisha shule zilizopo mbali kukosa walimu. Utali alisema hayo jana
alipofungua baraza la madiwani.
Alisema
shule zilizofanya vibaya kwenye matokeo ya darasa la saba ni zilizopo
mbali na barabara kuu na zenye upungufu wa walimu.
Mkuu
huyo wa wilaya ambaye kitaaluma ni mwalimu alisema anafahamu mbinu na
ujanja wanaofanya baadhi ya walimu wanaotaka kufundisha shule za
barabarani.
“Mwalimu
atakayekuja na kimemo cha kiongozi, ama cheti cha ndoa au ugonjwa na
kuomba afundishe shule iliyopo kando mwa barabara kuu usikubali
kumhamisha, tutumie madaktari tuwapime tujue hayo maradhi yao,” alisema Utali.
Mwenyekiti
wa halmashauri hiyo, Jonas Van Zeland alimtaka mkurugenzi kuwafuatilia
walimu watoro na wanaoshindwa kukaa jirani na shule wanazofundisha kwa
madai kuwa mazingira siyo rafiki.
Mkurugenzi
wa halmashauri hiyo, Kyomba alisema katika matokeo ya darasa la saba
mwaka huu, Wilaya ya Mvomero imeshika nafasi ya sita kimkoa na shule
zilizofanya vibaya ni zenye uhaba wa walimu.
Alisema
atahakikisha anafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye shule hizo na
kuwaomba wazazi, walezi na viongozi wengine wa kata na vijiji, pamoja na
madiwani kumpa ushirikiano.
chanziblog.
Comments