Licha
ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), kuwataka mawakili
wake wasijihusishe na chochote baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha
kufuta rufaa yake, mawakili hao wamepeleka maombi kuiomba mahakama hiyo
kumpa mteja wao muda wa kupeleka notisi ya kusudio la kukata rufaa.
Kutokana na hali hiyo, Lema anatarajiwa kufikishwa mahakamani hapo ili kujua hatima ya maombi ya rufaa yake.
Desemba
2, mwaka huu, mahakama hiyo ilifuta rufaa ya mbunge huyo kutokana na
kukatwa nje ya muda, huku mawakili wake wakitakiwa kuwasilisha kusudio
la kukata rufaa ndani ya siku 10.
Hatua
hiyo ilikuja baada ya uamuzi wa maombi ya marejeo ya mwenendo na uamuzi
wa mahakama ya chini kutupwa na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha na Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Sekela Moshi, Novemba 11, mwaka huu.
Wakili
wa Lema, Sheck Mfinanga, jana alisema wamepeleka maombi mahakamani hapo
wakiiomba impe mteja wao muda wa kupeleka notisi ya kusudio la kukata
rufaa na kusikiliza rufaa hiyo ya maombi ya dhamana.
“Tumepeleka
maombi mahakamani ili impe Lema muda wa kupeleka notisi ya kusudio la
kukata rufaa na kusikiliza rufaa yake. Maombi hayo yanatarajiwa
kusikilizwa na Jaji Dk. Modesta Opiyo,” alisema Mfinanga.
Lema
ambaye anashikiliwa kwa zaidi ya mwezi mmoja katika Gereza Kuu la
Kisongo, mjini Arusha, alikamatwa Novemba 2, mwaka huu, nje ya viwanja
vya Bunge mjini Dodoma na kufikishwa mahakamani mjini Arusha, Novemba 8,
mwaka huu, akikabiliwa na mashtaka ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. John
Magufuli.
Naibu
Msajili wa Mahakama hiyo, Angero Rumisha, alisema mahakama hiyo
imeifuta rufaa hiyo kwa sababu wakata rufaa waliikata nje ya muda.
Kutokana
na sababu hizo, mahakama hiyo ilikubaliana na pingamizi la awali
lililowasilishwa na mawakili wa Serikali, Paul Kadushi na Matenus
Marandu, walioomba mahakama hiyo isisikilize rufaa hiyo kwa sababu
imekiuka matakwa ya sheria, yanayotaka kutolewa kwa kusudio la kukata
rufaa kabla ya rufaa yenyewe.
Novemba
28, mwaka huu, rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa kwa Jaji Mfawidhi wa
mahakama hiyo, Fatuma Masengi, lakini ilishindikana baada ya mawakili wa
Serikali kuweka pingamizi.
Kwa
mujibu wa mawakili hao, mawakili wa Lema walikuwa wamekiuka matakwa ya
sheria yanayowataka kutoa notisi ya nia ya kukata rufaa badala ya kukata
rufaa yenyewe.
Katika
shauri hilo, Lema anawakilishwa na mawakili Adam Jabir, John Mallya,
Sheck Mfinanga na Faraji Mangula wakati upande wa Jamhuri unawakilishwa
na Kadushi na Marandu.
chanzo;mpekuziblog.
Comments