Alhajj Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya ufunguzi wa masjid
Muhammad (S.A.W) uliopo Fujoni Mzambarauni, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa
wa Kaskazini Unguja.
Akitoa nasaha zake kwa waumini wa Kiislamu wa Fujoni na vijiji vya
karibu, Alhajj Dk. Shein aliwasisitiza waumini hao kwamba kamwe
haitakuwa jambo jema msikiti kuwa chanzo cha mizozo na migongano kwani
msikiti ni nyumba ya Mwenyezi Mungu.
Alhajj Dk. Shein aliwataka waumini hao kuufanya msikiti huo kuwa
sababu ya watu kuzidi kuwa wamoja na kushikamana pamoja na kuendeleza
masuala ya dini huku akiwataka kutafuta uongozi madhubuti wa msikiti
huo.
Katika nasaha zake hizo, Alhajj Dk. Shein alieleza kusikitishwa kwake
na tukio lililofanywa na baadhi ya waumini wa Kiislamu hivi karibuni
huko kisiwani Pemba la kuchoma moto msikiti, kuiba mashine ya
kupandishia maji sambamba na baadhi ya waumini kubaguana katika baadhi
ya misikiti.
Aidha,, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa katika historia ya Uislamu,
misikiti imetoa mchango mkubwa katika kuuendeleza Uislamu kama chemu
chemu muhimu ya elimu katika fani mbali mbali za dini.
Vile vile, Alhajj Dk. Shein alisema kuwa misikiti ina mchango muhimu
katika kuwaunganisha wanajamii wanaosali pamoja na huwapelekea kujuana
na kushirikiana katika masuala mbali mbali na kusisitiza umuhimu wa
kuitunza misikiti ukiwemo msikiti huo mpya ambao una sifa zote.
Aliwaeleza Waumini hao kuwa ni jukumu lao wakiwa wazazi na walezi
kuwalea watoto katika maadili mema na mafundisho ya dini na kusisitiza
kuwa ulinzi wa watoto ni pamoja na kuwapa elimu, ili wajue mazuri na
mabaya sambamba na kuwapatia hifadhi ya maisha yao kwa kuwaepusha na
vitendo vya udhalilishaji na unjanjasaji.
Akiendeleza nasaha zake, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa kuwapatia
watoto elimu ni jukumu la kila mzazi, hivyo wazazi pia wanapaswa kuwa
ushirikiano walimu kwa kila hali ili wapate moyo wa kuitekeleza kazi yao
ambayo inajulikana kuwa ni ngumu.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwataka waumini wa dini ya Kiislamu
kuyatumia mafunzo ya Bwana Mtume (S.A.W) ili kuiepusha jamii na
mifarakano kwa kuimarisha umoja, kwani umoja ni nguvu.
Alhaj Dk. Shein alisema kwua kila mmoja kwa nafasi yake ajue ana
wajibu wa kuhakikisha jamii inakuwa salama dhidi ya vitendo vya
udhalilishaji wa watoto na kinamama pamoja na vitendo vyote vya uhalifu
ili jamii iendelee kuishi kwa mani.
“ Tushirikiane katika kuvikabili vitendo vinavyosababishwa na
kumongonyoka kwa maadili, malezi na utamaduni wetu tulioachiwa na wazee
wetu”,alisema Alhajj Dk. Shein.
Aidha, Alhaj Dk. Shein aliwataka Waumini wa Dini ya Kiislamu, kila
wanapopata wasaa waendelee kukumbushana umihumu wa kujiepusha na
makatazo ya Mwenyezi Mungu ili kujikinga na adhabu zake na kuyafanya
mambo yatakayowapa faida hapa duniani na huko akhera waendako.
Katika hotuba yake kwa Waumini hao, Alhajj Dk. Shein aliwaahdi kwamba
maombi yao yamepokewa na yatafanyiwa kazi na kuwataka kuendelea kuwa na
subira kwa yale mambo ambayo yanaweza kuchelewa katika utekelezaji kwa
mashirikiano ya Mwakilishi wa Jimbo hilo Balozi Seif Ali Idd..
Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wale
wote walioshiriki katika ujenzi wa msikiti huo azidi kuwafunguliwa
milango ya riziki bna watilie baraka katika kufanya shughuli zao.
Nae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwakilishi wa
Jimbo la Mahonda Alhajj Balozi Seif Ali Idd, alieleza juhudi
zilizochukuliwa katika kuhakikisha msfadhili wa ujenzi wa msikiti huo
anapatikana ikiwa ni pamoja na kutumiza ahadi yake ya kutafuta mfadhili
wa msikiti huo.
Alhajj Seif Idd aliwaeleza wananchi wa Fujoni kuwa kila muumini wa
dini ya Kiislamu ana haki ya kusali msikiti huo tena bila ya kuingiza
ubaguzi wa aina yeyote zikiwemo itikadi za kisiasa kwani hiyo ni nyumba
ya Mwenyezi Mungu kila mmoja ana haki kuitumia.
Nao wananchi wa Shehia ya Fujoni katika risala yao walieleza furaha
yao kwa kujengewa msikiti huo mpya ambapo walieleza kuwa hapo kabla
msikiti uliokuwepo ulikuwa haukidhi haja kutokana na udogo wake,
uchakavu sambamba na kwenda masafa marefu kufuata misikiti kwa ajili ya
sala za Idd na Ijumaa.
Katika risala hiyo iliyosomwa na Ustadhi Salmin Mbarouk, wananchi hao
walitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Balozi Seif kwa kuchukua
juhudi katika kutekeleza ahadi yake ya kutafuta mfadhili wa ujenzi wa
msikiti huo na kumpongeza mfadhili huyo ambapo pia walitumia fursa hiyo
kutoa maombi yao kwa Rais.
Mapema Sheikh Othman Maalim akitoa mawaidha katika ufunguzi huo
alieleza umuhimu kwa waislamu kujenga misikiti sambamba na kuendeleza
utamaduni wa kutoa sadaka kwa lengo la kupata fadhjila za Mwenyezi Mungu
na kufuata mienendo ya Mtume Muhammad (S.A.W).
Sheikh Othman Maalim alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Mfadhili
wa msikiti huo Ali Buwardy pamoja na msimamizi wa ujenzi wa msikiti huo
Bwana Yakoub Othman huku akieleza jinsi Allah (SW) anavyochukia wale
wanaotumia kinyume fedha za ujenzi wa misikiti.
Nae Sheikh Fadhil Soraga alisisitiza umuhimu wa waislamu kujenga
misikiti pamoja na kuepuka mifarakano na migogoro katika kuiendesha
msikiti hatua ambayo haileti tija kwa waislamu na uislamu wenyewe huku
akieleza haja kwa waumini kuwa na tabia njema itakayompwekesha Allah
(S.W)
Viongozi mbali mbali wa Serikali, viongozi wa dini ya kiislamu,
wananchi na wageni kutoka ndani na nje ya Zanzibar walihudhuria katika
ufunguzi huo wa masjid Muhammad (S.A.W).
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
chanzo; zanzibar24.
Comments