Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati alipokutana na Mabalozi wa
nchi hizo Ikulu mjini Zanzibar hivi leo, Dk. Shein alizipongeza nchi
hizo kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria ambao umekuwa
chachu katika kuimarisha juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kujileta maendeleo.
Akizungumza na Balozi wa Cuba katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
anaemaliza muda wake wa kazi hapa nchini, Jorge Luis Lopez Tormo, Ikulu
mjini Zanzibar, viongozi hao walisisitiza haja ya kuendelea kuimarisha
uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili hizo.
Katika Mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema kuwa Cuba ina historia
kubwa katika juhudi za kuiunga mkono Zanzibar kwenye sekta za maendeleo
hasa sekta ya afya kwani tokea mwaka 1964 nchi hiyo imekuwa ikileta
madaktari wake kuja kufanya kazi hapa Zanzibar.
Alieleza kuwa mbali ya madaktari hao kuja kufanya kazi kwa kutoa
huduma ya afya kwa jamii hapa nchini, Cuba imekuza uhusiano wake kupitia
sekta hiyo kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kuanzisha chuo cha Udaktari ambacho tayari kimeshaanza kuza matunda kwa
kutoa Madaktari Wazalendo.
Aidha, alisema kuwa mbali ya ushirikiano wa sekta ya afya alieleza
haja ya kuanzishwa ushirikiano katika sekta ya utalii kutokana na Cuba
kupiga hatua kubwa katika sekta hiyo.
Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka kwa
ndugu zao wa Cuba kutokana na nchi hiyo kujiimarisha kwenye sekta ya
utalii sambamba na vyanzo vyake vya utalii yakiwemo maeneo ya kitalii
likiwemo eneo maarufu la ukanda wa kitalii la ‘Varadero’.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa ushirikiano huo pia,
utahusisha mji Mkongwe wa Zanzibar na ule mji Mkongwe wa Havana ambao
yote kwa pamoja ina historia kubwa pamoja na vivutio kadhaa vya kitalii
ndani yake.
Pia, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kwa mara nyengine tena kutoa mkono
wa pole kwa kifo cha kiongozi shupavu na mpigania haki za wanyonge
marehemu Fidel Castro, na kumtumia salamu Rais Raul Castro za kumtakia
afya njema yeye na wananchi wa Cuba ili waendelee kulijenga taifa hilo.
Dk. Shein alisisitiza haja kwa nchi hiyo kuunga mkono azma ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwasomesha madaktari wazalendo
katika vyuo vikuu vya afya nchini humo kupitia kada maalum za udaktari
kwa kiwango cha elimu ya juu kwa ufadhili wa SMZ.
Nae Balozi Jorge Luis Lopez Tormo alimuhakikikishia Dk. Shein kuwa
Cuba inathamini sana uhusiano na ushririkiano wa kihistoria kati yake na
Zanzibar na kuahidi kuendelea kuudumisha.
Balozi huyo wa Cuba kuwa miradi yote ya maendeleo inayoishirikisha
nchi yake itaendelezwa kwa juhudi kubwa huku akimueleza Dk. Shein kuwa
nchi yake itafarajika kwa kuwepo ushirikiano katika sekta ya utalii.
Balozi Tormo alisema kuwa kwa mwaka huu pekee, Cuba imeweza kupokea
watalii wapatao milioni tatu na nusu na kukiri kuwa mfanano wa miji
mikongwe ya Zanzibar na Havana unaweza kuwa chachu katika kukuza utalii
kwa pande zote mbili.
Mapema, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi Mdogo mpya wa Oman,
Ahmed Bin Humoud Al Habsi, ambapo alitumia fursa hiyo kuipongeza Oman
kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati zake za kukuza
uchumi na kuimarisha maendeleo.
Dk. Shein alieleza kuwa miongoni mwa juhudi zilizochukuliwa na Oman
katika kuisaidia Zanzibar ni pamoja na ujenzi wa Chuo cha Afya kilichopo
Mbweni pamoja na fedha taslim kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya Kiwanda
cha Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, msaada wa gari kwa ajili ya viongozi
wa Serikali na misaada mengine ambayo nchi hiyo imeshawi kuitoa.
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Sultan Qabous Bin
Said Al Said na Serikali yake kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na
alimtaka Balozi huyo wa Oman amfikishie salamu zake kwa kiongozi huyo.
Nae Balozi Ahmed Bin Humoud Al Habsi, ambaye amechukua nafasi ya
Balozi Mdogo wa Oman aliemaliza muda wake wa kazi hapa Zanzibar, Ali
Abdulla Al Rashdi alieleza kuwa Oman itaendeleza uhusiano na ushirikiano
wake kati yake na Zanzibar na kupongeza hatua za maendeleo zilizofikiwa
hapa nchini.
Aidha, Bin Mahmoud alisema kuwa Serikali ya Oman inatambua juhudi
zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa
Dk. Shein za kujiletea maendeleo hivyo, Oman itaendelea kuziunga mkono
juhudi hizo ili Zanzibar izidi kupata mafanikio.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
chanzo; zanzibar24.
Comments